Mkurugenzi Mkuu NSSF akutana na Waziri Mkuu Uganda

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:25 PM Jan 28 2025
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Masha Mshomba, amekutana na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Uganda, Robinah Nabbanja Jijini Dar es Salaam.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Masha Mshomba, amekutana na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Uganda, Robinah Nabbanja Jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Masha Mshomba, amekutana na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Uganda, Robinah Nabbanja Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza mara baada ya kikao jana, Mshomba amesema Robinah Nabbanja amefika nchini kwa lengo kuhudhuria Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika ambapo mbali na mkutano huo aliona ni vizuri kukutana na NSSF kwa lengo la kufahamu mambo kadhaa kuhusu utendaji wa Mfuko ikiwa pamoja na suala la ukuaji wa thamani ya Mfuko, uwekezaji, usajili wa wanachama wa sekta binafsi na sekta isiyo rasmi na ulipaji wa mafao ya wanachama ili kupata uzoefu.

“Kama tunavyofahamu nchi yetu ya Tanzania imepata heshima kubwa kuwa mwenyeji wa mkutano mkubwa wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika na Mhe. Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Uganda amefika hapa nchini kwa lengo la kuhudhuria mkutano huo, lakini ameona ni vizuri kuja kukutana na NSSF kwa lengo la kufahamu masuala kadhaa ya utendaji ikiwemo uwekezaji unaofanywa na NSSF, ulipaji wa mafao na masuala mengine ya huduma ikiwemo ushirikiano kati ya NSSF Tanzania na ile ya Uganda' na kwa kweli tumezungumzia hayo ambayo aliomba tuyazungumzie na tumemueleza kwa mfano uwekezaji wetu katika dhamana za Serikali, uwekezaji kwenye miundombinu mfano wa Daraja la Nyerere Kigamboni, Kiwanda cha Sukari cha Mkulazi kule Morogoro na miradi mengine ambayo NSSF imewekeza ikiwa ni pamoja na ile ya majengo” amesema Mshomba.

Mshomba pia amemueleza Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Uganda kuwa NSSF ipo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, hususani kitengo cha Hifadhi ya Jamii pamoja na Benki Kuu ya Tanzania na Ofisi ya Msajili wa Hazina kwenye masuala ya uwekezaji.

Vile vile, Mshomba amesema Mfuko umeimarika sana katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilipoingia madarakani.

“Katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Rais wetu mpendwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, NSSF imepata mafanikio makubwa ya utendaji hii inatokana na juhudi kubwa sana ya serikali yake katika kuvutia wawekezaji nchini," amesema Mshomba.

Alisema kwa sababu NSSF inawafikia waajiri na wajiriwa katika sekta binafsi na pia sekta isiyo rasmi, hivyo wawekezaji wanavyokuja nchini, inapelekea ongezeko la wanachama, inaongeza waajiri, na hivyo kuongeza michango. Aidha, uwekezaji na mapato yanayotokana na uwekezaji yamekuwa yakiongezeka.

Mshomba amemueleza Robinah Nabbanja kuwa NSSF imeruhusiwa kuwekeza nje ya nchi katika eneo la Afrika Mashariki, pia katika eneo la SADC, ambapo kwa uwekezaji huo utasaidia kuongeza mapato ya NSSF kupitia uwekezaji huo.

“Katika uwekezaji huo tulioruhusiwa kuwekeza nje ya nchi, NSSF tumekuwa tukishirikina na Mifuko mingine ya Hifadhi ya Jamii, mfano wenzetu wa NSSF Uganda tunapofikiria kuwekeza katika HISA nchini Uganda ni lazima tushirikiane nao kupata uzoefu wao katika soko la HISA la Uganda," amesema Mshomba.

Kwa upande wa ushirikiano katika ya Mifuko miwili ya NSSF Tanzania na NSSF Uganda ni mzuri kwani NSSF Tanzania imekuwa ikiwapa ushirikiano mzuri NSSF Uganda hasa wanapokuja kuwekeza Tanzania, ambapo wao wameanza kuwekeza katika dhamana za Serikali kwa muda mrefu.

“ Mheshimiwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Uganda amefurahi sana kuona ushirikiano uliopo na wenzetu wa NSSF  Uganda na akatoa rai kuwa ni vizuri tukaendeleza ushirikiano huo kwa sababu si tu unajenga hizi taasisi mbili bali unajenga nchi na unaimarisha uhusiano katika nchi na nchi kitu ambacho ni muhimu hasa tunapofikiria kuendeleza Jumuiya ya Afrika Mashariki na hilo amesisitiza sana na akaahidi atakaporudi nchini Uganda ataweka msisitizo katika hilo.” ameongeza Mshomba

Kwa upande wake, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Uganda, Robinah Nabbanja aliipongeza NSSF kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kuwahudumia wanachama na Taifa kwa ujumla na kuomba ushirikiano uendelee kwa maslahi mapana ya nchi zote mbili.