Rais wa Jamhuri ya Liberia, Joseph Boakai ni miongoni mwa marais wa Afrika 19 ambao wameshawasili jijini Dar es Salaam kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati, ulioanza jana, Januari 27, 2025 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere.
Rais Boakai amepokelewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Shariff Ali Shariff alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam.
Mbali na Marais hao wapo pia Makamu Marais wa Afrika, Mawaziri na Naibu Mawaziri Wakuu wanaowawakilisha Marais wa nchi zao pamoja na mawaziri wengine wa nchi za Afrika.
Mkutano huo ulianza kwa Mkutano wa ngazi ya Mawaziri na hii leo Januari 28 unafanyika Mkutano Wakuu wa Nchi ikiwa ni kilele cha Mkutano huu.
Aidha, Mkutano huo unatarajiwa kupitisha Azimio la Dar es Salaam, lenye kuonesha dhamira ya pamoja ya viongozi wa Afrika kuhakikisha upatikanaji wa nishati Afrika ni wa uhakika, nafuu, na endelevu kwa maendeleo ya bara la Afrika.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED