UBALOZI wa Kenya uliopo Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), umeshambuliwa na waandamanaji wenye hasira wakipinga mzozo unaoendelea mashariki mwa nchi hiyo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Kenya, Korir Sing’oei ametaja hatua hiyo iliyofanywa na waandamanaji kama ghasia dhidi ya Taifa la Kenya.
Aidha waandamanaji hao waliolenga balozi za nchi wanazozituhumu kushirikiana na Rwanda katika kuunga mkono waasi wa M23, wamefikia hatua hiyo baada ya kuonesha kutoridhishwa na hali ya usalama mashariki mwa DRC.
M23 ni kikundi cha waasi kinachotokana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kilichoundwa mwaka 2012.
Kikundi hiki kinajulikana kwa kupigana dhidi ya serikali ya DRC na kinajikita hasa katika eneo la Mashariki mwa Kongo, hasa katika mkoa wa Kivu Kaskazini na sasa wameikali Goma.
Jina "M23" linatokana na neno la kifaransa 'Mouvement du 23 mars' yaani March 23 Movement vuguvugu la Machi 23.
Jina hili linarejerea mkataba wa amani uliofikiwa mwaka 2009 ambao haukutekelezwa ipasavyo, na ndipo kikundi hiki kilipoanzishwa.
Kundi la M23 lilianzishwa mwaka 2012 wakati karibu wanajeshi 300 wengi wao wakiwa wanachama wa zamani wa Chama cha Kitaifa cha Ulinzi wa Wananchi (CNDP) walipoiasi serikali ya DRC, wakitaja hali mbaya ya jeshi na serikali kutokuwa tayari kutekeleza agizo hilo la Mkataba wa Machi 23, 2009 uliokuwa wa makubaliano ya amani.
M23 kinajumuisha wapiganaji wengi ambao ni sehemu ya makabila mbalimbali, na kikundi hiki kinatajwa kupata msaada kutoka kwa nchi jirani kama Rwanda, ingawa Rwanda imekana sera hizo.
Mapigano kati ya M23 na jeshi la serikali ya DRC yamepelekea mizozo mingi na madhara kwa raia, ikiwa ni pamoja na kuhamasisha watu wengi kukimbia makazi yao.
Kikundi hiki kimekuwa na ushawishi mkubwa katika siasa za eneo hilo, huku ripoti zikionyesha kuwa kinaweza kuwa na lengo la kutafuta udhibiti wa rasilimali za asili za Kongo, kama vile madini.
Hali hiyo imezidi kukwaza juhudi za amani katika eneo hilo na kuleta changamoto kubwa kwa usalama wa kikanda.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED