EWURA yahimiza wadau wa umeme Singida kutoa huduma bora

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:56 PM Jan 28 2025
EWURA yahimiza wadau wa umeme Singida kutoa huduma bora.
Picha:Mpigapicha Wetu
EWURA yahimiza wadau wa umeme Singida kutoa huduma bora.

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Kanda ya Kati leo imekutana na wadau mbalimbali wa sekta ya umeme mkoani Singida ili kupokea maoni, ushauri na changamoto zinazowakabili kwa lengo la kuimarisha utoaji wa huduma zinazokidhi viwango vya ubora.

Mhandisi Mwandamizi wa  EWURA Kanda ya Kati, Nicholaus Kayombo, akitoa mada kuhusu umuhimu wa leseni za usanikishaji mifumo ya umeme kwa wadau hao, amewakumbusha mafundi umeme kuhakikisha wanawapatia nakala ya cheti cha kukamilisha kazi wateja wao pindi kazi za usanikishaji zinapokamilika.

Amesema Mamlaka imebaini kuwa suala hilo halizingatiwi ipasavyo jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Akitoa maoni yake, mmoja ya washiriki, Mkandarasi Ernest Msengi amewaomba EWURA, kufuatilia kwa kina huduma zinazotolewa na mafundi umeme mkoani humo ili kujiridhisha kuhusu ubora wa vifaa vinavyotumika kufunga mifumo ya umeme kwani ameeleza kuwa, kumekuwapo matumizi ya  vifaa vyenye ubora hafifu kwa baadhi ya wateja hali inayotishia usalama wa mali, mazingira na afya za watu.

Msengi ameongeza kuwa, kwa kiasi kikubwa mafundi wanaotumia vifaa hafifu ni wale wasiokuwa na leseni hivyo ametoa rai kwa EWURA kuongeza hamasa ili mafundi umeme wote waombe leseni na kutoa huduma kwa mujibu wa sheria,kanuni na taratibu zilizowekwa.

Wadau walioshiriki ni pamoja na wawakilishi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya,Manispaa, Shirika la Nyumba la Taifa, TEMESA, TANESCO, VETA, EWURA CCC, wakandarasi wa umeme na mafundi umeme wenye leseni na wasiokuwa na leseni za EWURA pamoja na baadhi ya wanafunzi wanaosomea usanikishaji wa mifumo ya umeme.