BAADA ya kupata ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Copco FC na kutinga hatua ya robo fainali ya Kombe la FA, Kocha Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic, amesema kazi iliyobaki sasa ni kushinda kila mchezo wa mbele yao kwa timu yoyote ile watakayokutana nayo, bila kujali ni ndogo au ya daraja la chini.
Akizungumza juzi, baada ya kumalizika kwa mchezo huo uliopigwa Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam, Ramovic, alisema tangu mwanzo aliwaambia watu kuwa hadharau timu yoyote, hivyo kipigo hicho kimewastahili Copco na ataendelea na utaratibu wa kutoidharau timu yoyote ile, iwe kwenye Ligi Kuu au Kombe la FA.
"Tumecheza vizuri kwenye huu mchezo, tumeingia hatua ya robo fainali, hatuangalii timu ndogo, timu ya daraja la chini, au tumepangiwa na mpinzani wa aina gani, tunajiangalia wenyewe.
"Watu wasidhani kuwa tumefunga mabao kirahisi, unaona jinsi gani ilivyokuwa timu nzuri na iliziba mianya kipindi chote cha kwanza, cha pili matokeo yaliamuliwa kwa sisi kubadilisha mfumo , pia uwezo na kipaji cha mchezaji mmoja mmoja, tutajaribu kuendelea na makali haya kwa yeyote yule atakayekuja bila kujali ipo chini ya msimamo wa Ligi Kuu au ipo daraja la chini Kombe la FA," alisema kocha huyo.
Ushindi huo unakuja wiki moja tu baada ya kushindwa kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ilipolazimishwa sare dhidi ya MC Alger ya Algeria na kuishia nafasi ya tatu ya msimamo wa Kundi A.
Kocha Mkuu wa Copco, yenye maskani yake jijini Mwanza, Lucas Mlingwa, alisema mpango wao kwa kiasi kikubwa ulifanikiwa, kilichotokea kupigwa mabao yote hayo ni kupungua kwa umakini wa wachezaji wake.
"Mimi naona imeenda kama tulivyo 'plan', tupunguze eneo la kucheza, hasa nyuma pale katikati ili tujue wanashambulia kutokea wapi, na tulifanikiwa, tuliamua wapite pembeni si ndani, kipindi cha kwanza tulifanikiwa, hakuna bao lolote lililopitia kati, walilolipata lilikuwa la kona," alisema kocha huyo.
Alisema ubora wa wachezaji wa Yanga na uchanga waliokuwa nao, ndiyo ulioamua mechi hiyo, huku akiwasifu vijana wake kwa kufuata maelekezo aliyowapa.
"Kipindi cha pili kilichotugharimu ni umakini ulipungua, kukaa kwenye mpango kwa dakika 90, kwa wachezaji wadogo hawa ilikuwa ngumu sana, wakawa na fatiki kichwani, lakini mpango wetu leo umekwenda sawa na hata ukiangalia mabao karibuni yote yamefungwa kutokea pembeni na si ndani, nimefurahi kwanza tumefanya kile tulichokubaliana na kimefanyika," alisema.
Yalikuwa ni mabao ya Shekhan Ibrahim, Prince Dube, Maxi Nzengeli, Duke Abuya na Mudathir Yahaya, yakitosha kuiangamiza timu hiyo inayocheza, 'First Legue.'
Wakati Yanga inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na pointi 39, Copco FC, iliyoshuka msimu uliopita kutoka Champioship, inashika nafasi ya sita kwenye msimamo wa First League, Kundi B , ikiwa na pointi tano kwa michezo saba iliyocheza, katika ligi yenye makundi mawili na kila kundi likiwa na timu nane.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED