Rais Samia ataka vijana kugombea ubunge, udiwani

By Jenifer Gilla , Nipashe
Published at 08:22 AM Jan 25 2025
RAIS Samia Suluhu Hassan.
Picha:Mtandao
RAIS Samia Suluhu Hassan.

RAIS Samia Suluhu Hassan amesisitiza vijana kugombea ubunge na udiwani katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, mwaka huu.

Aliandika hayo juzi  katika ukurasa wake X akitilia mkazo hoja iliyoandikwa na mtumiaji wa mtandao huo, aliyejulikana kwa jina la Thomas Kibwana akiwakumbusha vijana kushiriki uchaguzi huo.

Msisitizo huo umekuja wakati utafiti wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Elimu, Sayansi na Utamaduni wa mwaka 2022, ukionesha kuwa asilimia 40 ya vijana wenye sifa hawashiriki kwenye uchaguzi.

Akichangia hoja hiyo, Rais Samia aliwakumbusha vijana kuwa kushiriki Uchaguzi Mkuu ikiwamo kugombea nafasi za uongozi ni sehemu ya wajibu wao.

Rais Samia alisema uhuru na ulinzi wa mapinduzi ya nchi unajengwa na kuwapo kwa vijana wenye uthubutu hasa katika kuwania nafasi mbalimbali za uongozi.

“Huu ni ushauri mzuri hasa wakati huu kuelekea uchaguzi mkuu. Sehemu ya wajibu wa vijana wetu ni kushiriki mchakato wa uchaguzi, ikiwamo kugombea nafasi za uongozi na kutumikia ipasavyo wanapopata nafasi,” alisema.

Hoja ya Kibwana ililenga kuwasisitiza vijana kuchukua fomu na kuwania nafasi za udiwani na ubunge bila kujali vyama wanavyoviwakilisha.

“Vijana chukueni hizo fomu mwaka huu mgombee nafasi za udiwani na ubunge. Haijalishi upo chama gani wewe chukua fomu gombea,” aliandika Kibwana.

Vilevile, Rais Samia alishukuru kwa kupata nafasi ya kujifunza kwa vitendo kwa miaka mitatu katika ulingo wa siasa akisisitiza kuwa, msingi wa siasa na uongozi ni utumishi na kumtanguliza Mungu.

“Ukishatanguliza hilo pamoja na kuomba mkono wa Mwenyezi Mungu, mengine yatakwenda vizuri, ikiwamo mikakati ya utekelezaji wa unayokusudia,” alisema.

Aliandika hivyo akimshukuru mtumiaji wa mtandao X, AshaDi aliyemsifia kuwa ni mtaalam wa siasa na demokrasia nchini.

“Ila utani pembeni, Dk. Samia Suluhu Hassan ni mtaalamu wa siasa na masuala ya siasa,” aliandika.

Utafiti uliofanywa na Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID) mwaka 2020 ulionesha kuwa ni asilimia 64 pekee ya vijana walioshiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa na ulikuwa upigaji kura, na asilimia ndogo zaidi wakijitokeza kama wagombea kwenye nafasi mbalimbali za uongozi.

Kwenye takwimu hizo, asilimia 35 ilikuwa vijana waligombea nafasi za wenyeviti wa kijiji, nafasi za udiwani (asilimia 27) na nafasi za ndani ya vyama vyao vya kisiasa (asilimia 24), huku asilimia 14 wakihudumu kama wajumbe wa mabaraza ya serikali za mitaa.