Vijue vifutio vya ndoto unazoota usiku

By Flora Wingia , Nipashe
Published at 09:39 AM Jan 26 2025
AI
Picha: AI
AI

KARIBU tena msomaji wangu tuendelee na mada yetu kuhusu kufutwa au kuchafuliwa kwa ndoto zetu tunazoota usiku tumelala.

Kumbuka ndoto unayoota inahusiana sana na mipango yako. Ni kitu halisi kinachoanzia kwenye ulimwengu wa roho. Mungu huongea na sisi sana kupitia ndoto ili kuifanya hiyo ndoto iwe wazi.

Ndoto ni mjumbe anayekuletea habari ya kile kinachoendelea kwenye ulimwengu wa roho, ule usioonekana kwa macho ya damu na nyama. Yaani ukoje wewe katika ulimwengu wa roho.

Ndoto ni kile ambacho Mungu amekupa kukifanya duniani. Lakini adui hufuta na kuzichafua ndoto zako ili usifanikiwe katika maisha yako.

Mungu husema nasi katika ndoto. Na katika maandiko yake amesema na watu mbalimbali wakiwemo manabii. Kwa mfano aliwaambia Haruni na Miriamu, “Sikilizeni basi maneno yangu; Akiwapo nabii kati yenu, Mimi BWANA nitajifunua kwake katika maono, Nitasema naye katika ndoto. Hesabu 12:6).

Hebu sasa tuende zaidi tuangalie ndoto zetu zilizochafuliwa, zinafutwaje kwenye ulimwengu wa roho? Cha kwanza unapoota ndoto unalishwa chakula. Hicho kinaitwa ni chakula kichafu kilichochafuliwa.

Unapoota ndoto unalishwa chakula hiyo ni kifutio cha ndoto. Mara nyingi watu wengi wanaoota kula vyakula kwenye ndoto inakuwa ni vyanzo vya kufuta ndoto zako zilizo wazi.

Hata ukiota ndoto ya kitu kizuri, Mungu anakuonya jambo fulani huwezi kuelewa chochote, ukiamka asubuhi umesahau. Lakini utagundua uliota ndoto ya kula chakula ndotoni. 

Hiyo inakuwa ndoto zako zimechafuliwa. Ni ujumbe ambao umechafuliwa. Ni sawa na umeletewa barua lakini juu ya hiyo barua mtu akaandika vitu vyake vingine akaichafua.

Unaota ndoto mwanzoni kilikuwa ni kitu kizuri kisha mwishoni kitu kinatokea kama vile amekula chakula na vyote vizuri vinafutika. Na hii haitokei tu katika kusahau ndoto bali hata kusahau mambo ya ibada nyumba za dini.

Mtu anaingia kwenye ibada anasikiliza vizuri mafundisho ya Mungu na yanamgusa, lakini akitoka hapo, maadui wameshafuta. Hapo kuna mtandao wa vyakula vya kichawi ulivyokula ndotoni unafuta. Mapepo na chachawi, hawa ndio wahudumu wazuri wa kuchafua kabisa ndoto au kuzifuta. 

Futio mojawapo ni kulishwa vyakula kwenye ndoto. Ukishalishwa chakula, tayari mfumo wa kufuta vile vitu vizuri unafuta. Wewe utakachokumbuka ni ndoto ya kula chakula.

Kumbe adui ameshajua kuwa huyu mtu anataka atambue siri fulani ambayo Mungu anasema naye kupitia ndoto. Adui analeta hiyo unashangaa amefuta.

Kifutio kingine cha pili cha ndoto ni ndoto za vitisho. Yaani unatishwa kwenye ndoto. Inawezekana ukawa na ndoto njema kabisa ambayo inakutahadharisha jambo, lakini hizi zingine zimetokea za vitisho unashtuka unaamka. Unashangaa zile ndoto ulizoota zote zimefutika!

Lakini adui alitumia mbinu ya kukutisha kwenye ndoto.  Mungu anakupa ujumbe mzuri lakini adui analeta picha ya kukutisha, anafuta ndoto nyingine zote nzuri za hatma yako.

Unaamka unakumbuka ni kama vile ulikuwa unakabwa usiku, unakimbizwa na watu usiowajua. Kumbe hapo ni adui alikuja kukutisha ili kufuta ule ujumbe wa Mungu wa ndoto zako njema!

Na hujui cha kufanya, wewe unajua tu ulikimbizwa kwenye ndoto, utaanza kukemea majinamizi, unaishia hapo. Kumbe kuna mbinu iliyotumika ya kufuta ujumbe kamili ambao Mungu alikuwa anakupa kwenye ndoto.

Kifutio cha tatu, ni kuota ndoto unafanya zinaa yaani, unazini kwenye ndoto. Anatumika mwanamke wa kichawi au mwanaume wa kichawi. Unakuta umefikia kitu cha upenyo mzuri adui analeta kifutio cha ndoto hiyo mbaya.

Unashangaa alfajiri uliishia kufanya mapenzi kwenye ndoto. Unajiuliza, mbona kuna kitu nilikipata kwenye njozi halafu alfajiri naanza kuota ndoto za ajabu ajabu ndio nashtuka? Unasema naikumbuka ile ya mwisho ya zinaa kwenye ndoto.

Hicho ni kifutio, adui ametumia ile picha ya mwisho kufuta ndoto nzuri. Ni sawa na mtu umepata ujumbe wako mzuri, unatoka pale umechangamka, unakutana na vitu njiani vinakufutia kila kitu. 

Hizo ndoto ungezikumbuka ujasiri ungeongezeka ndani yako. Ila unazokumbuka ni za kubakwa na kadhalika. Ndoto nyingi ambazo Mungu alikuletea zimefutwa. Mjue sana Mungu upate maarifa kufuta ndoto mbaya!

Mpenzi msomaji, bila shaka umepata picha kuhusu yale yanayojiri kwenye ndoto usiku. Hadi wiki ijayo. Una maoni? Ujumbe 0715268581.