WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dk. Damas Ndumbaro, ametaja maeneo manne yenye kadhia kubwa kwenye mikoa 11 iliyofikiwa na Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (MSLAC).
Ameyataja maeneo hayo kuwa ni migogoro ya ndoa, migogoro ya ardhi, mirathi na ukatili wa kijinsia.
Akizindua jana kampeni hiyo mkoani Kigoma, itakayovifikia vijiji 240 ndani ya siku tisa, Dk. Ndumbaro alisema katika mikoa 11, wananchi 775,119 wamefikiwa na kupokea na kusikiliza migogoro 3,162.
Alisema katika awamu hii kampeni hiyo itafanyika mikoa sita na hivyo kuifikia mikoa 17, huku akibainisha kuwa kwa Mkoa wa Kigoma eneo ambalo linaonekana kuwa na kadhia ni tatizo la uraia.
Kutokana na changamoto hiyo, Dk. Ndumbaro, amemwagiza Kamishna Jenerali wa Uhamiaji kuweka banda la uhamiaji ili wananchi wasikilizwe na wenye haki ya kupatiwa uraia wapewe.
Kadhalika, amemwagiza Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Kigoma kuwa kila eneo ambalo kampeni itafanyika kuwe na banda la watu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ili kusikiliza kero na migogoro ya wananchi na wanaohitaji hati wapate.
Alisema moja ya changamoto iliyoko kwenye mirathi ni watu kuogopa kuandika wosia wakiamini ni kujichuria kifo wakati kuna watu wamewaandikia wosia na bado wapo hai.
“Wosia si kifo ni matakwa yako wewe endapo Mungu atakuchukua unataka familia yako iishi vipi wakati haupo. Hapa sisi wote tutakufa haijulikani ni lini, sasa ikitokea unataka nyumba au shamba lako liwe vipi, wosia ni jambo muhimu kama unaitakia mema familia yako na ni la wote wanawake na wanaume,” alisema.
Kuhusu kamati za msaada wa kisheria wilaya na mikoa, alisema maeneo mengi hazifanyi kazi ipasavyo zimelala hivyo, kupitia kampeni hiyo, elimu inayotolewa ni kuzifufua ili msaada wa kisheria uratibiwe ngazi ya mikoa hadi mitaa.
Waziri huyo alisema zaidi ya asilimia 54 ya sheria zote zimebadilishwa lugha kutoka Kiingereza kwenda Kiswahili.
“Rais Samia ametuletea elimu ya msaada wa kisheria na msaada wa kisheria kwa wale wenye changamoto bure kwa wote wenye uhitaji ili kupata haki zao. Uzinduzi huu niliofanya Kigoma mikoa mingine sita itakayofikiwa na kampeni awamu hii ni Katavi, Tabora, Mtwara, Geita na Kilimanjaro,” alisema.
Naye Mbunge wa Kigoma Mjini, Kilumbe Ng’enda, alisema kampeni hiyo ni muhimu kwa wananchi wa Kigoma kwa kuwa wengi wao wanapoteza haki kwa kukosa msaada wa kisheria.
“Moja ya haki zinazosumbua watu ni haki za kiraia, kuna watu wanakosa baadhi ya haki za kisheria kwasababu wanashindwa kujua utaratibu wa kukana uraia wa mzazi mmoja ambaye si raia wa Tanzania kunasababisha leo akose kitambulisho cha NIDA, leseni ya udereva, biashara na kukimbizana na vyombo vya dola,” alisema.
Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Dk. Rashid Chuachua, alisema kampeni hiyo itakuwa chachu ya maendeleo na itaweka mazingira wezeshi kwa wananchi kufanya shughuli zao bila hofu na wananchi wapo tayari kupokea msaada huo wa kisheria.
Awali, akizungumza kwa niaba ya Waziri Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima, Naibu Katibu Mkuu, Amon Mpanju, alisema kampeni hiyo inakwenda kutatua migogoro mingi kwa jamii.
Kadhalika alisema inakwenda kusaidia kujua namna ya kuzifikia haki zao na inatekeleza mpango wa kukabiliana na ukatili wa wanawake na watoto.
Mwakilishi wa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora kutoka Zanzibar, Yusfa Abdalla Said, alisema ofisi hiyo inatarajia kuzindua kampeni hiyo katika mikoa ya Unguja na Pemba Februari, mwaka huu.
Mwakilishi wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Baraka Mbwilo, alisema TLS inamuunga mkono Rais Samia kwa kuanzisha kampeni hiyo ili kuwafikia wananchi kutoa msaada wa kisheria.
Alitoa wito kwa wananchi kujitokeza kuhudumiwa na kupatiwa msaada wa kisheria, huku akiwaomba mawakili wasikilize vizuri wananchi na kuchambua ili kuangalia sheria gani zinapaswa kutumika kwenye mgogoro husika na kuzipeleka kwenye mahakama kuzisimamia ili wapate haki zao.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Kitaifa ya Ushauri ya Msaada wa Kisheria, Saulo Malauli, alishauri huduma hiyo iwe endelevu kwenye wilaya na mikoa kwa kuweka utaratibu baada ya kampeni angalau mara tatu kwa mwaka ili kuwafikia wananchi wengi na kutatua changamoto za kisheria zinazowakabili.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED