JK aipa PPAA changamoto kuokoa fedha za serikali katika miradi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:20 PM Jan 25 2025
Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Kikwete akipokelewa na Mwenyekiti wa Mamlaka ya Rufani, Jaji Mstaafu Sauda Mjasiri alipotembelea banda la Mamlaka hiyo wakati wa uzinduzi wa maonesho ya Wiki ya Sheria yaliyoanza leo tarehe 25 Januari, 2025
Picha: Mpigapicha Wetu
Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Kikwete akipokelewa na Mwenyekiti wa Mamlaka ya Rufani, Jaji Mstaafu Sauda Mjasiri alipotembelea banda la Mamlaka hiyo wakati wa uzinduzi wa maonesho ya Wiki ya Sheria yaliyoanza leo tarehe 25 Januari, 2025

Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne,Dk. Jakaya Kikwete ameipa Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) changamoto ya kuangalia jinsi ununuzi wa umma unavyoweza kuokoa fedha za umma na kuhakikisha kuwa Serekali inapata thamani ya fedha katika miradi yake inayoitekeleza.

Kikwete ametoa changamoto hiyo wakati alipotembelea banda la PPAA katika maonesho ya Wiki ya Sheria yaliyoanza tarehe 25 Januari, 2025 katika viwanja vya Nyerere Square Jijini Dodoma.



“Wakati nilipokuwa Rais kuna halmashauri moja ilijenga jengo lake kwa kutumia shilingi milioni 15 kwa jitihada zao wenyewe, lakini wakaambiwa kwamba wasiendelee na utaratibu ule lazima zabuni itangazwe, baada ya zabuni kutangazwa wakanionesha nyumba iliyojengwa kwa milioni 45,” alisema Dk. Kikwete.



Hivyo kuna umuhimu wa wadau wa sekta ya ununuzi wa umma kuhakikisha kuwa Sheria ya ununuzi wa umma inasaidia kupatika kwa thamani halisi ya fedha katika miradi mbalimbali.



Awali Afisa Mwandamizi wa PPAA, Stanley Jackson alimweleza Dk. Kikwete kuwa kwa kipindi cha takribani miaka minne, PPAA imeweza kushughulikia mashauri 162 yaliyotokana na michakato ya Ununuzi wa Umma ambapo katika mashauri hayo, PPAA ilizuia utoaji tuzo kwa zabuni 35 zenye thamani ya takribani bilioni 583.6 kwa wazabuni wasio na uwezo wa kifedha pamoja na wale waliokosa sifa za kitaalamu za kutekeleza zabuni husika. 



“Hatua hiyo iliepusha utekelezaji usioridhisha wa miradi unaosababisha upotevu wa fedha za umma na kuchelewesha maendeleo stahiki kwa wananchi,” alisema Jackson. 



Pamoja na mambo mengine, Jackson aliongeza kuwa Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imekamilisha utengenezaji wa moduli ya kuwasilisha na kushughulikia rufaa na malalamiko kwa njia ya kielektroniki (Complaint and Appeal Management Module) katika Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST).  



Jackson aliongeza kuwa, kukamilika kwa Moduli hiyo kutawawezesha wazabuni kuwasilisha kwa njia ya kielektroniki malalamiko na rufaa zitokanazo na michakato ya ununuzi wa umma kwa Taasisi Nunuzi na Mamlaka ya Rufani pasipo kulazimika kutembelea ofisi husika.



“Ili kuwawezesha wazabuni na watendaji wa taasisi nunuzi kutumia moduli hiyo, PPAA kwa kushirikiana na PPRA imeandaa mafunzo ya matumizi ya moduli ya kushughulikia malalamiko na rufaa kwa njia ya kielektroniki yatakayoambatana na tamko rasmi la kuanza kwa matumizi ya moduli hiyo.  



…..Mafunzo haya yanawalenga wazabuni na watendaji wa taasisi nunuzi wa mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Kagera, Musoma, Geita na Simiyu.  Mafunzo yatafanyika kuanzia tarehe 4 - 6 Februari, 2025 Jijini Mwanza katika Ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) uliopo Capripoint,” alisema Jackson 



Mamlaka ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) ni taasisi inayojitegemea chini ya Wizara ya Fedha iliyoundwa kwa mujibu wa Kifungu cha 112 cha Sheria ya Ununuzi wa Umma Namba 10 ya mwaka 2023.  PPAA imepewa kisheria jukumu la kupokea na kusikiliza malalamiko na rufaa zinazotokana na michakato ya Ununuzi wa Umma na kufungiwa kwa wazabuni (blacklisting of tenderers) kushiriki katika michakato ya Ununuzi wa Umma na Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA).



Maadhimisho ya wiki ya sheria yameongozwa na Kauli Mbiu: “Tanzania ya 2050: Nafasi ya Taasisi zinazosimamia Haki Madai katika kufikia Malengo Makuu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo”.