Simba yatoa fundisho FA

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 08:43 AM Jan 27 2025
SAFI HIYO...
Augustine Okejepha (kushoto), akimpongeza Ladack Chasambi, kwa kuifungia timu yao bao la pili wakati Simba ikiibuka na ushindi wa mabao 6-0 dhidi ya Kilimanjaro Wonders kwenye mechi ya raundi ya tatu ya michuano ya Kombe la FA
Picha: Mpigapicha Wetu
SAFI HIYO... Augustine Okejepha (kushoto), akimpongeza Ladack Chasambi, kwa kuifungia timu yao bao la pili wakati Simba ikiibuka na ushindi wa mabao 6-0 dhidi ya Kilimanjaro Wonders kwenye mechi ya raundi ya tatu ya michuano ya Kombe la FA

TIMU ya Simba, imesonga mbele Kombe la FA, baada ya kuichakaza Kilimanjaro Wonders mabao 6-0 katika mchezo wa raundi ya tatu ya michuano hiyo kusaka bingwa atakayeiwakilisha nchi kwenye Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao.

Ushindi huo ulikuwa ni kama kuwajibu watani wao wa jadi ambao Jumamosi iliyopita iliikandika Copco FC mabao 5-0, kwenye uwanja huo huo wa KMC Complex uliopo Mwenge, Dar es Salaam ikiwa ni mechi nyingine ya kombe hilo.

Simba ilianza biashara asubuhi, kabla ya dakika moja kutimia, walipoanzisha mpira bila wapinzani wao kugusa wakaukwamisha mpira wavuni.

Alikuwa ni Valentin Nouma, ambaye baada ya gonga mbili, aliambaa na mpira kwenye wingi ya kushoto na kupiga krosi iliyounganishwa kwa mguu na Velentino Mashaka sekunde ya 23 tu tangu mpira kuanza.

Ladack Chasambi alifunga bao la pili dakika ya nne ya mchezo baada ya wachezaji wa Simba kupasiana karibu na lango la wapinzani wao, mfungaji awali alipiga pasi ya kisigino kwa Awesu Awesu, ambaye naye alipeleka pembeni, wingi ya kulia, kabla ya David Kameta kupiga krosi iliyounganishwa naye.

Bao la tatu liliwekwa ndani ya nyavu na beki wa Kilimanjaro Sebastian dakika ya tisa, baada ya kukabiliwa na shuti la Valentine Nouma.

Mpira ulitoka kwa Mzamiru Yassin, ambaye alimpenyezea Joshua Mutale, aliyepiga pasi ya kisigino kwa Nouma, ambaye shuti lake lilimbabatiza beki huyo na kumpoteza maboya kipa, Farances Kizuguto.

Mutale alifunga bao la nne dakika ya 20, baada ya kipa Kizuguto kuupiga pembeni kwa mabeki wake, lakini wakachelewa kuupitia na kuujaza wavuni.

Mabao hayo yalidumu hadi mapumziko, huku kipa wa Simba Ally Salim, akiwa kama yuko likizo licha ya kujaribiwa na mipira miwili ya hatari, alipookoa shuti la  Hamis Ramadhani, kabla ya Playgod Nassari kukosa bao la wazi, baada ya kuukuta mpira uliorudishwa na Nouma kwa kipa wake, lakini haukwenda mbali.

Shuti lake akiwa karibu na lango, halikuwa na shabaha, mpira ukatoka nje.

Kipindi cha pili, angalau vijana wa Kilimanjaro Wonders, walionekana kuamka, lakini ni baada ya kufungwa bao la tano mara tu baada ya kuanza kipindi hicho, dakika ya 48 lililowekwa wavuni kwa kichwa na Steven Mukwala, likiwa ni bao pekee lililofungwa kwa staili hiyo kwenye mechi hiyo.

Mpira ulianzia nyuma kwa Abdulrazack Hamza, ambaye aliupeleka pembeni kwa Duchu, aliyeambaa kwenye wingi ya kulia na kupiga krosi ya juu, mfungaji akiruka na kuunganisha, akimwacha kipa, Kizunguto, akiruka bila mafanikio.

Mukwala alikuwa ameingia kuchukua nafasi ya Mashaka, ambapo mbali na mchezaji huyo, wengine walioingia ni Edwin Balua badala ya Augustine Okejepha, Kelvin Kijili naye akiingia badala ya Hamza.

Baada ya mabao hayo, wachezaji wa Simba walionekana kuridhika na kupunguza kasi yao, hali iliyowafanya Kilimanjaro Wonders kuanza kujinafasi kwa kupigiana pasi fupifupi nyuma, kabla ya kupiga mipira mirefu pembeni ambapo mara kadhaa walifanikiwa kuipenya ngome ya Simba, lakini wachezaji wao, Miraji Sallah, Joseph Sekue, Joachim Limbu, hawakuwa makini.

Mchezaji mwingine aliyeingia kipindi cha pili, Balua, alifunga bao la sita, dakika ya 79 kwa shuti kali la umbali ambalo wengi walidhani kipa Kizuguto angedaka, lakini ulimparaza mikononi na kutinga wavuni.

Baada ya bao hilo timu zote hazikuonekana kama kuna kitu zinasaka tena, zaidi ya kucheza kwa kupoteza muda ili mechi imalizike.