Yanga ikubali kujifunza Simba mechi za maamuzi kimataifa

By Mhariri Mtendaji , Nipashe
Published at 10:11 AM Jan 20 2025
Yanga ikubali kujifunza Simba mechi za maamuzi kimataifa.
Picha:Mtandao
Yanga ikubali kujifunza Simba mechi za maamuzi kimataifa.

KLABU ya Yanga imeshindwa kusonga mbele kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kumaliza mechi za Kundi A, ikiwa nafasi ya tatu juzi.

Yanga ilimaliza ikiwa na pointi nane na kuziacha MC Alger ya Algeria ikiwa ya pili na pointi zake tisa, huku kinara wa kundi akiwa ni Al Hilal Omdurman ya Sudan iliyomaliza na alama 10.

Katika mchezo huo dhidi ya MC Alger uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, pamoja na kutawala kwa asilimia 69, na kuwaacha wapinzani wao wakiwa na asilimia 31, bado hawakuwa na mbinu mbadala za kuwafungua na kupata angalau ushindi wa bao moja ambao ungewavusha.

Tunadhani bado Yanga haijafahamu jinsi gani ya kucheza michezo kama hii ya kimataifa, ambayo haihitaji zaidi mbwembwe na kutawala mechi, zaidi ya mbinu, mikakati, kujituma na ubinifu wa kupata matokeo chanya.

Katika michuano hiyo, ilionekana Yanga ilitaka kucheza mechi hizo kama inavyocheza dhidi ya Fountain Gate, Dodoma Jiji, KMC, ambapo muda wote inatawala mchezo huku ikisubiri makosa ya wapinzani wao ili kuwaadhibu. Badala yake MC Alger haikutengeneza makosa badala yake ilitengeneza mfumo wa kuzuia ambao ulikuwa mwiba mchungu kwa Yanga.

Tulitegemea kuona Kocha Mkuu wa timu hiyo, Sead Ramovic, akiwaanzisha Pacome Zouzoua na Clatous Chama katika mchezo huo kwa sababu wanaonekana ni wabunifu na wana uwezo wa kuwafungua wapinzani zaidi kuliko walioanza.

Mechi ya juzi hakuna ambacho Yanga ilihitaji zaidi ya kufunga mabao, hivyo tangu dakika ya kwanza ingekuwa na wachezaji ambao wangeweza kusababisha madhara langoni mwa mpinzani.

Pacome ni mchezaji mwenye uwezo wa kukokota mpira kwa umbali mrefu na kuingia nao ndani ya eneo la hatari, hivyo angesababisha madhara makubwa, pia Chama hana haja ya kuelezewa sana kwani ni mtaalam wa mechi kama hizi za maamuzi, kazi hii akiifanya sana wakati akiwa na timu ya Simba.

Tunaamini katika kusaka maendeleo itakuwa si vibaya kwa Yanga kujifunza kwa timu zilizofanikiwa, na kwa hapa nchini katika michuano hiyo hususan hatua muhimu kama hiyo ya maamuzi kwa mechi ya mwisho ni Simba. Ni kwa sababu wanajua jinsi ya kucheza mechi hizo, wanacheza kwa mikakati, kuheshimu wapinzani na si kwa presha sana.

Ndiyo maana utaona kwenye mechi za maamuzi kama hizo, Simba huanza taratibu na mara nyingi hutanguliwa kufungwa bao, lakini wachezaji wake wanatulia na kurudisha magoli, wakati mwingine kupata na la ushindi.

Kwa misimu saba, Simba imetinga robo fainali sita, nne za Ligi ya Mabingwa na mbili Kombe la Shirikisho, wakati Yanga ikiwa na robo fainali moja Ligi ya Mabingwa na Shirikisho moja.

Desemba 23, 2018, Simba iliifunga Nkana FC mabao 3-1, katika mchezo wa maamuzi ili kutinga hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika na msimu huo huo, ilitinga robo fainali kwa kuifunga AS Vita Machi 16, 2019.

2021, Simba iliifunga Al Merrikh ya Sudan mabao 4-1 na kutinga hatua ya robo fainali kwenye mchezo wa maamuzi, iliongoza kundi lililokuwa na Al Ahly ya Misri, Machi 18, 2023, ikaiadhibu Horoya FC ya Guinea mabao 7-0, na Machi 2, 2024, iliichakaza Jwaneng Galaxy mabao 6-0, mechi zote hizo zikiwa ni za maamuzi ya kutinga robo fainali, Ligi ya Mabingwa Afrika.

Somo hili kwa Simba walilipata kwenye michezo ya makundi 2019, walipokuwa wakipigwa mabao mengi wakijifanya kucheza kwa swaga, ikapigwa 5-0 dhidi ya AS Vita na idadi kama hiyo dhidi ya Al Ahly.

Hata Mabingwa wa kihistoria wa michuano hii, Al Ahly, siku zote haionekana kucheza soka la kuvutia machoni, lakini wamekuwa ndiyo wanaokwenda kutwaa ubingwa, hapo pia kuna la kujifunza.