KATIKA jamii ya Kitanzania, mtaani tunakotajiwa kuwapo mzigo mkubwa wa majukumu ya kutafuta riziki, kuna kundi kubwa la vijana waliozama katika shughuli inayojulikana kama ‘Machinga.
Huo ni uchuuzi mdogo ulioajiri kundi kubwa la vijana na hasa mijini, ingawa vijijini nako si haba hivi sasa!
Wanaozama katika eneo hilo la uchuuzi, moja ya bidhaa zao kuu ni uuzaji wa maji ya kunywa.
Kutokana na hali halisi ya maisha, pia kimazingira, baadhi ya mikoa nchini kunashuhudiwa kuwapo joto kali, ikiwamo majiji kama ya Dar es Salaam na Tanga, hata tunapovuka bahari kuhamia Unguja na Pemba, kote kuna joto kali, hasa katika misimu husika.
Katika hilo, kundi kubwa la watu linahitaji maji kwa kiu, hata kuwa mtindo wa maisha ya kisasa, huku aina nyingine ya kumiminika, kuna juisi.
Niseme katika msimu huu wa matunda, wapo wanaouza matunda na wapo wanaotengeneza juisi. Kumekuwapo matunda ya aina mbalimbali kwa wingi katika masoko, hivyo watu hufanya biashara ya kuuza juisi na matunda yake.
Sasa kuna ubunifu wa ziada ambao unanipa maswali magumu kiafya na kiusalama, ndani ya joto hilo kali linalowaletea watu kiu; chupa za maji zilizotumika, zinasuuzwa na kutumika tena, wateja nao wanajitosa kununua maji hayo.
Ndicho walichonacho baadhi ya wauzaji juisi, kama walivyo wenzao wa maji, wamekuwa wakiuza zilizowekwa katika chupa za plastiki zenye maandishi mbalimbali ya bei, kinywaji kikiuzwa kati shilingi 500, hadi 200 hata kufika shilingi 100.
Hao wauzaji pia, juisi na maji yao unakuta chupa hawanunui katika maduka, wengi wanaokota katika vyanzo kama kuvizia penye sherehe, wanazikusanya na kuzitumia kwa ajili ya kuweka juisi na maji hayo.
Pia, wapo wanaookota chupa mitaani na kuwapelekea wauza juisi na maji kwa ajili ya kufanyia biashara. Hapo usalama wa afya ya mtumiaji juisi na maji unasimamia wapi?
Inasikitisha, kwa sababu kuna mbadala salama, hivi sasa yapo maduka mengi yanayouza vifungashio vya kila biashara.
Hivyo, inatakiwa tuboreshe biashara kupitia vifungashio hivyo. Zipo glasi na vikombe ambavyo hutumiwa na wateja, kisha wanavyotupa.
Niseme, wafanyabiashara wanaweza kutumia vifungashio hivyo na sio kutumia chupa ambazo baadhi zinakuwa zimetupwa katika maeneo yasiyofaa, halafu zinaokotwa na kupelekwa kufanyia kazi hiyo.
Pia ufike hatua, mjasiriamali aone kasoro, penye huduma za kukaa, zikitumika glasi zinaweza kutumika, zinaoshwa na kuendelea kutumiwa, tofauti na chupa hata zinapooshwa.
Si ajabu, hata kama zimeoshwa bado mapungufu huwa yanakuwapo kwa chupa zilizookotwa.
Hivyo, hapo inatupatia nadharia kwamba, chupa za kuokota ni mitihani kwa afya ya watumiaji, iwe maji au juisi.
Labda tutasafiri mbali na hilo, katika namna ya kujiondoa nayo na sababu iko wazi kuwa imebeba masilahi ya watu, ndugu zetu machinga.
Ni mahali sahihi kwa mamlaka za kiserikali, hasa zinazohusika na afya kuweka mkakati kwa kushirikiana na dola kuu, kukabili hatari hizo kabla hatujafika pabaya.
Katika mfano mdogo, hata tunavyopiga kelele katika mazingira fulani kuhusu magonjwa ya kuambukiza, maana inazama kwa mazingira hatarishi ya maradhi ya kuambukizana kwa namna hiyo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED