MAHAKAMA ya Wilaya ya Iringa imeahirisha kesi ya mauaji ya aliyekuwa Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kilolo, Christina Kibiki hadi Februari 17 itakapotajwa tena kutokana na upelelezi wa kesi hiyo kutokamilika.
Akiomba kuahirishwa kwa kesi hiyo juzi, Wakili wa Serikali, Atupele Makoga, alisema kuwa wanaomba kesi hiyo ipangwe siku nyingine ili waweze kukamilisha upelelezi wa kesi hiyo.
Wakili wa utetezi, Barnabas Nyalusi kutoka kampuni ya mawakili ya BLS Attorney &Partner, aliiambia Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Wilaya ya Iringa, kuwahimiza upande wa Jamhuri kuharakisha upelelezi wa kesi hiyo kutokana na siku 90 walizopewa kisheria kukabia kuisha.
Wakili Nyalusi alidai mbele ya mahakama kuwa kesi hiyo inasikilizwa na kufuatiliwa na jamii kwa ukaribu na kwamba ni vema mchakato wa upelezi ukakamilika haraka ili ianze kusikilizwa.
Kutokana na maombi hayo ya upande wa Jamhuri, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya ya Iringa, Adelina Ngwaya, aliahirisha kesi hiyo.
Waliofikishwa mahakamani hapo ni pamoja Boniphace Ugwale, ambaye ni Diwani wa Kata ya Nyanzwa Kilolo, Kefa Wales, Silla Kimwaga, Willy Chikweo na Hedikosi Kimwaga kwa pamoja wanashtakiwa kumuua Christina Kibiki.
Washtakiwa hao wanadaiwa kutenda kosa hilo Novemba 12, 2024 katika Kijiji cha Ugwachanya, Wilaya ya Iringa Vijijini.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED