SAKATA la mgogoro wa ardhi katika eneo la Shule ya Msingi na Sekondari Zavala, Kata ya Buyuni, jijini Dar es Salaam limechukua sura mpya baada ya baadhi ya wananchi kuamua kwenda mahakamani kufungua kesi kudai wanachoita "haki".
Ni umauzi uliofikiwa baada ya Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, kuwapa mwezi mmoja kubomoa nyumba zao walizojenga katika eneo hilo linalodaiwa kuwa ni shule hizo.
Mkuu wa Wilaya alitoa amri ya kuwataka wananchi wa eneo hilo kubomoa nyumba zao Januari 23, mwaka huu wakati wa kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Wiki iliyopita amri hiyo ya mkuu wa wilaya ilianza kutekelezwa, huku baadhi ya wananchi wakidai inafanyika kinyume cha maagizo yake kwa kuwa mazungumzo kati ya pande mbili hayajafikia mwisho.
Mmoja wa waathirika aliyebomolewa nyumba zake tatu, Richard Amos alisema kutokana na tukio hilo, anakusudia kufungua kesi katika Mahakama Kuu ya Tanzania kudai haki yake.
Amos alidai kuwa katika kikao chao na mkuu wa wilaya, walishindwa kuelewana kutokana na kusimamia upande mmoja na wao kukosa nafasi ya kujitetea kuhusiana na jinsi walivyopata eneo hilo, hivyo yeye na wenzake wamekubaliana kwenda mahakamani.
"Mkuu wa wilaya hayuko juu ya sheria, sisi tumeamua kwenda mahakamani kufungua kesi ili mahakama iweze kutafsiri sheria," alidai Amos.
Akizungumzia mgogoro huo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya Ilala, Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilala, Charangwa Makwiro, alisema wananchi walionunua viwanja katika eneo hilo wametapeliwa.
Charangwa alisema kuwa baada ya kikao cha wananchi na mkuu wa wilaya, walitakiwa kuonana naye ili awasaidie katika masuala ya kisheria, hata hivyo, wananchi hao hawakwenda baada ya kuwa na msimamo wa kwenda mahakamani.
Shabani Haruna, mmoja wa waathirika wa ubomoaji huo, alidai "uamuzi wa kubomoa nyumba za watu ni ubabe wa madaraka wa mtu mmoja, hivyo tunakusudia kwenda mahakamani kutafuta haki."
Haruna alidai kuanza kubomoa nyumba za watu ilhali kulikuwa na mazungumzo yaliyokuwa yanaendelea kati yao na mkuu wa wilaya, kumewashangaza.
Katibu wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Ilala, Mtiti Jilabu, alimwomba Mkurugenzi wa Jiji hilo, Elihuruma Mabelya, kushughulikia haraka mgogoro wa ardhi ulioibuka katika eneo hilo ambalo inadaiwa mmiliki wake halali ni George Chawala.
Mgogoro huo umeibuka baada ya mmiliki wa sasa wa eneo hilo, Shabani Haruna, maarufu Mapete, anayedaiwa kulinunua kutoka kwa Chawala kisha kukata viwanja na kuwauzia watu mbalimbali ambao wamejenga makazi ya kudumu.
Mapete alidai kuwa alilinunua kutoka kwa Chawala zaidi ya miaka mitatu iliyopita, naye Chawala alilinunua kwa Musa Nyemba mwaka 2000, kulingana na hati ya mauziano aliyoitoa mnunuzi wa pili.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED