KESI ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroine kilo 34.89 inayomkabili aliyekuwa Kocha wa Makipa wa Klabu ya Simba, Muharami Sultani na wenzake watano, imeanza kunguruma Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu, washtakiwa wakikana mashtaka.
Mmiliki wa Kituo cha Michezo cha Cambianso kilichoko Tuangoma, Kigamboni mkoani Dar es Salaam, Kambi Zubery amekana kuongoza wenzake kufanya biashara ya dawa za kulevya na amekana kukamatwa mpakani Horohoro, Tanga akitaka kutorokea Kenya.
Hayo yalibainishwa jana mbele ya Jaji Godfrey Isaya wakati washtakiwa wakisomewa mashtaka na maelezo ya awali ya kesi inayowakabili.
Akisoma mashtaka, Wakili wa Serikali Tully Helela alidai washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka manane; kati ya mwaka 2016 na Novemba 2022, maeneo ya Dar es Salaam na Mkuranga, wote wanadaiwa kuongoza genge la uhalifu na kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroine.
Ilidaiwa kuwa Oktoba 27, 2022, huko Kivule, Ilala mkoani Dar es Salaam, washtakiwa walikutwa wanasafirisha dawa za kulevya aina ya heroine kilogramu 27.10.
Ilidaiwa pia kuwa Novemba 4, 2022, eneo la Kamegele, Mkuranga, kwa pamoja walikutwa wanasafirisha kilogramu 7.79 za dawa za kulevya aina ya heroine.
Mshtakiwa Kambi anakabiliwa na mashtaka matano kati ya manane ya kutakatisha fedha, ikidaiwa alijipatia magari matano aina ya Tata wakati akijua mali hizo zimetokana na mazalia ya kosa la kuongoza genge la uhalifu.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Kambi, Sultani, Maulid Mzungu, maarufu Mbonde, Said Matwiko, John Andrew maarufu Chipanda ambaye ni mfanyakazi wa Cambiasso na Sara Joseph ambaye ni mke wa Matwiko.
Akisoma maelezo ya awali, Wakili Tully alidai maofisa wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kuzuia Dawa za Kulevya (DCEA), wakiwa kwenye doria maeneo ya Kivule, walipata taarifa ya watu wanasafirisha dawa za kulevya.
Alidai mtoa taarifa aliwaongoza nyumbani kwa mshtakiwa Matwiko na kundi lingine lilielekea Kitunda Magole kwa mshtakiwa John.
Ilidaiwa katika kufanya upekuzi nyumbani kwa Saidi, walikuta pakiti 27 zilizodhaniwa kuwa dawa za kulevya, mshtakiwa Saidi na Sarah walikamatwa na vielelezo vilipelekwa kwa Mkemia kwa ajili ya uchunguzi ambako ilibainika ni dawa za kulevya aina ya heroine.
Ilidaiwa pia upekuzi ulifanyika nyumbani kwa washtakiwa wengine wote na nyumbani kwa Maulid kulikutwa pakiti nane za dawa za kulevya.
Mshtakiwa Kambi alidai kuwa wakati wa upekuzi unafanyika nyumbani kwake, hakuwapo na zilichukuliwa Sh. milioni tisa na gari na kwamba si kweli kwamba simu nne zilikutwa nyumbani kwake.
Alidai hakukamatwa katika Mpaka wa Horohoro, Tanga akitaka kukimbilia Kenya bali alikamatwa maeneo karibu na Horohoro.
Mshtakiwa Kambi alikana kuwafahamu washtakiwa wengine wote lakini mshtakiwa wa pili na watatu walikubali kwamba wao ni ndugu na mshtakiwa wa nne alikubali kwamba mshtakiwa wa sita ni mke wake.
Washtakiwa wote walikubali majina yao kwamba ni sahihi lakini walikana maelezo mengine yote kuhusiana na biashara ya dawa za kulevya.
Katika kesi hiyo upande wa Jamhuri una jumla ya mashahidi 30 na vielelezo 90 kwa ajili ya kuthibitisha mashtaka dhidi ya washtakiwa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED