CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimetambulisha wagombea wake wa nafasi ya urais huku kikiweka wazi mikakati mitano ya kuendelea kubaki madarakani huku kipaumbele kikiwa kuondoa tatizo la ajira kwa vijana kwa kuanzisha programu maalum.
Akitaja mikakati hiyo jana jijini hapa kwenye sherehe za miaka 48 ya CCM, Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan, alisema kwa miaka mitano ijayo watabaini changamoto mpya na kunyumbulika kwa wakati kuzitatua.
“CCM imebaini changamoto ya tatizo la ajira kwa vijana na inatambua hii ni changamoto ya dunia nzima, tumeanza na mabadiliko kwenye sera ya elimu kama nguzo ya kuwajenga kiujuzi na kiutaalamu watoto wetu,” alisema.
Alisema ujuzi huo utawawezesha kunufaika na fursa ajira kwenye maeneo yao.
Pia alisema serikali inaweka programu na mipango mbalimbali ya kuboresha mazingira ya biashara nchini ili kuvutia na kuwa na mitaji ya uwekezaji ndani na nje ya nchi ili waajiriwe na kujiajiri.
“Tunafanya jitihada za makusudi kufanya uwekezaji kwenye michezo, sanaa na burudani na uzoefu kutoka nchi zingine umeonekana sekta hizi zinatoa mchango kiuchumi na zinatengeneza ajira nyingi rasmi na zisizo rasmi,” alisema.
Pia alisema zinafanyika jitihada za kukuza ufanisi katika sekta ya utalii na kuimarisha uchumi wa buluu kwa kuwa zimeonesha uwezo mkubwa wa kutoa ajira kwa vijana.
“Serikali imeanzisha programu mbalimbali zenye lengo la kujiajiri mwenyewe na kuajiri wengine, kama programu ya jenga kesho iliyo bora (BBT) kwenye sekta za kilimo, mifugo, madini na nyuki, vijana wanajengewa uwezo wanapewa mitaji na nyenzo,” alisema huku akibainisha kuwa programu hizo ndio zinaonesha kesho ya CCM.
“Jambo jingine la kutuhakikishia kesho yetu ni kujenga jumuiya ya vijana ya CCM na kuwajenga vijana kiitikadi ili wajue vizuri siasa ya nchi yetu na misingi ya kuanzishwa CCM. Kesho salama ya chama chetu na nchi yetu itahakikishwa kwa vijana wetu kujengewa uwezo ndani na nje ya nchi ili kujipanga kitaasisi ili kupambana kwa hoja na yeyote mwenye hoja hasi,” aliongeza.
Alisema lazima Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) kuimarishwa kimkakati kwa kuwa ni hazina ya CCM kwa kuwajengea uwezo na kupikwa kiitikadi katika mazingira ya sasa.
Kadhalika, alisema kwa kuwa CCM inatekeleza ahadi zake anaamini wananchi wataendelea kuwapa dhamana ya kuongoza serikali zote mbili.
“Tukiangalia kazi tuliyoifanya kipindi hiki, tunaamini kuwa uchaguzi wa mwaka huu hali haitakuwa tofauti, watanzania wataendelea kutupa dhamana ya kuongoza serikali zote mbili,” alisema.
Alisema pamoja na hali hiyo, wasibweteke kwa kujiamini kuwa ni chama kikubwa na chenye matumaini makubwa kwenye uchaguzi ujao.
“Tunatimiza miaka 48 kwenye mwaka wenye vuguvugu la uchaguzi mkuu nchini. Tusiruhusu kunyemelewa na kiburi cha kuwabeza wapinzani wetu lakini tusiingiwe na pepo la kuwaogopa. Tuendelee kulinda heshima na imani tuliyopewa na wananchi kuliongoza taifa letu,” alisema.
Samia alisema CCM imejipanga kuendelea kutoa uongozi thabiti kwa ustawi wa taifa na haitabadili itikadi yake ya kuwatumikia watu wote na imani yake ya binadamu wote ni ndugu na Afrika ni moja.
“Kuaminika kwa CCM hakujatokea tu inatokana namna inavyoshughulikia matatizo ya wananchi na utekelezaji wa ahadi yake zilizomo kwenye ilani ya uchaguzi za kujenga uchumi imara, kutatua changamoto za kijamii na kujenga miundombinu mbalimbali ya biashara na uwekezaji, hii ni kete ya imani ya wanachama,” alisema.
Aidha, alisema huko waendako wananchi wataipima CCM kwa sera na mipango, kazi wanazofanya. Aliwataka wana CCM kuwafikia na kuwasikiliza wananchi na kutatua changamoto zao na CCM imejipanga na matumizi ya TEHAMA ili kurahisisha mawasiliano.
Pia alihimiza viongozi katika kuelekea uchaguzi mkuu waongeze kasi ya kuwatembelea wananchi na wanachama kwa kuwafahamisha namna serikali ilivyotekeleza ilani.
“Mwalimu (Julius) Nyerere aliwahi kusema Rais wa chama chetu anaweza kutoka chama chochote lakini Rais bora atatoka CCM. Nataka niwahakikishie wakati utakapofika kwa kushirikiana na wagombea hawa wenzangu walioteuliwa na timu nzima ya CCM tutapeperusha vyema bendera ya CCM na naimani wananchi watatupa dhamana ya kuendelea kuongoza, CCM Baba lao na Mama lao wengine bado wanafunzi wajifunze,” alisema.
Kuhusu uteuzi wagombea ubunge na madiwani, Rais Samia aliwahakikishia wanachama kwamba CCM itatenda haki katika kupata wagombea wanaotokana na CCM na wanaokubalika.
Naye Katibu Mkuu wa CCM na Mgombea Mwenza Mteule, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, alisema atatumia uwezo wake kusaidia kazi alizozianzisha Rais Samia na kuhakikisha hazirudi nyuma.
Pia alisema mafanikio ya utekelezaji ya Ilani ya CCM ya 2020, inampa jeuri ya kuwa tayari kuendelea kufanya kazi chini ya Rais Samia.
“Nina imani kuwa nitafanya kila lililo ndani ya uwezo wangu kuhakikisha kwamba kazi unayoifanya hairudi nyuma, kuhakikisha kwamba nakusaidia kwa nguvu na uwezo wangu wote,” alisema.
Alisema pia atashiriki kusaidia kuhakikisha kwamba kasi ya maendeleo ambayo Rais Samia ameyaanzisha yanazidishwa maradufu.
Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, alisema wanachama wanawajibu wa kudumisha mafanikio ya CCM kwa kuimarisha umoja na mshikamano.
“Wana CCM tuna wajibu wa kudumisha misingi ya chama chetu na kuzidi kuimarisha chama chetu kwa kuendelea kushika dola za serikali zote mbili na tunawajibu wa kuhamasisha wanachama wetu kujiandikisha kwenye daftari la wapigakura na wakati ukifika wanakwenda kuichagua CCM,” alisema.
Alisema mafanikio ya utekelezaji wa ilani kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar yanatosha wananchi kukiamini na kuchagua CCM katika uchaguzi mkuu ujao.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED