KATIKA mwaka wa fedha 2023/24 na 2024/25 serikali imewarasimishia ujuzi vijana 20,234 na kuwapa fursa ya kwenda kwenye vyuo mbalimbali kuongeza elimu watakayoitumia kujiajiri na kujiingizia kipato.
Hayo yalisemwa jana bungeni na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi, wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Latifa Juakali, aliyehoji serikali ina mpango gani wa kuwatambua vijana wenye ujuzi ambao hawatambuliki rasmi ili kuwaendeleza.
Alisema serikali imeendelea kuwatambua vijana wenye ujuzi ambao hawatambuliki kupitia kuboresha mazingira ya kisera ili kuwawezesha vijana kushiriki katika shughuli za maendeleo na kujitegemea kupitia Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana (2007) toleo la mwaka 2024, na Sera ya Taifa ya Ajira ya Mwaka 2008.
Alisema vijana 20234 walirasimishiwa ujuzi kwa kupata mafunzo kupitia kada mbalimbali ikiwamo useremala, ushonaji, uwashi na ufundi na wamekuwa wakitumika katika miradi ya serikali.
“Hata ujenzi wa miradi mikubwa ikiwamo Bwawa la Mwalimu Nyerere na SGR wale vijana walikwenda wakiwa hawana elimu na wamejifunza kupitia ujenzi na sasa tunawarasimishia ujuzi na wanakwenda kwenye vyuo mbalimbali kwa ajili ya kuongeza ujuzi na tutawatumia katika ukarabati,” alisema.
Alisema utekelezaji huo unafanyika kupitia programu maalum inayoitwa Recognition of prior learning na zaidi ya vijana 616 walirasimishiwa ujuzi na walipewa vyeti kwa ajili ya kutambulika kupitia programu ya BBT, vijana 500 walipata vyeti vya kutambuliwa ujuzi wao baada ya kupata mafunzo ya ziada na 234 walirasimishiwa ujuzi wa unenepeshaji wa mifugo kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Alisema pia inarasimisha na kutambua ujuzi wa vijana uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa elimu, wanabuni na kutekeleza programu maalum kupitia sekta zinazozalisha ajira kwa wingi kama vile sekta ya kilimo kupitia programu ya Jenga Kesho iliyobora (BBT), ujasiriamali na madini kupitia programu ya Mining for a better Tomorrow (MBT).
Serikali pia inaimarisha utoaji wa mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi wa ngazi za Stashahada na Shahada kupitia maboresho ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, toleo la mwaka 2023.
Alisema serikali pia inajenga miundombinu ya kimkakati inayochochea uchumi ambayo inakuza ujuzi na inachangia kuzalisha ajira, akitoa mfano wa ujenzi wa Bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere na barabara za mwendokasi (BRT).
Pia, inabuni na kutekeleza programu ya kukuza ujuzi ambayo inalenga kukuza ujuzi kwa nguvu kazi ya taifa mfano mafunzo ya kuongeza ujuzi kwa wafanyakazi waliopo kazini na wajasiriamali; na kuweka msisitizo kwenye matumizi ya TEHAMA katika kuzalisha fursa nyingi za ajira kwa vijana.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED