WAKATI joto likiendelea kupanda la kusitishwa kwa miradi ya afya, Shirika la Misaada ya Kimataifa (USAID), limejiondoa kwenye mitandao ya kijamii na kufunga tovuti yake, huku wafuasi wa Chama cha Demokratiki wakifanya maandamano na kupinga uamuzi wa Rais wa Marekani, Donald Trump kusimamisha shughuli zake kwa siku 90.
Aidha, kumekuwa na maoni tofauti kuhusu uamuzi huo, baada ya Mbunge wa Jimbo la Nzega Vijijini, Dk. Hamis Kigwangala, akipendekeza nchi za Afrika kuwekeza zaidi katika sekta ya afya ili kuwahakikishia wananchi wake wote huduma bora na sio kutegemea wafadhili.
Nipashe ilitembelea akaunti mbalimbali za USAID na kubaini kutokuwapo hewani tangu Februari 4, mwaka huu tovuti na kurasa za mitandao ya kijamii hazikuwa na maudhui yoyote na jana tovuti ilikuwa na taarifa kuhusu mpango wa kuwapumzisha wafanyakazi wake.
Kupitia ukurasa wake wa X, Dk. Kigwangala alisema muda wa kutegemea wafadhili umepita na kwamba ni lazima nchi hizo zibuni mbinu mpya na za kisasa za kugharamia afya za watu wake.
Alisema, kupungua kwa fedha za wafadhili katika sekta ya afya barani Afrika ni changamoto kubwa inayohitaji hatua za dharura kutoka kwa serikali za bara hilo.
“Muda wa kutegemea wafadhili umepita. Ni lazima tubuni mbinu mpya na za kisasa za kugharamia afya za watu wetu,” alisema Dk. Kigwangala.
Alisema ni muhimu kuwa na mkakati madhubuti kama wa bima ya afya kwa wote, kodi maalum za kulipia bima kwa watu wasio na uwezo pamoja na kuhakikisha kila mtu anakuwa na bima ya afya.
Dk. Kigwangala ambaye ni mtaalamu wa afya ya jamii mwenye Shahada ya udaktari wa binadamu na Shahada ya Uzamili ya afya ya jamii (MPH), alishauri kuwa na utaratibu mzuri wa matumizi ya rasilimali kwa uwazi, ubunifu na uwajibikaji ili kuboresha mfumo wa afya na kupunguza utegemezi wa misaada ya nje.
Kupitia akaunti zake hizo za kijamii, Dk. Kigwangala alipendekeza mbinu za kisasa za kugharimia afya za watu ikiwa ni pamoja kila Mtanzania kuwa na bima ya afya.
“Kwa Tanzania watu wasio na uwezo ni asilimia 26.4 sawa na watu milioni 16.3, kama hao watahitaji kuchangiwa na serikali, fedha Sh. trilioni 2.445 sawa na Sh.150,000 kwa kila mtu.
“Sheria ya bima ya afya kwa wote namba 13 ya mwaka 2023, kwenye kifungu cha tano, tayari inalazimisha kila Mtanzania kuwa na bima ya afya, bila kujumuisha watu wengi, mfumo unaweza kuwa dhaifu kifedha na kushindwa kufanikisha huduma bora kwa wote,” alisema Dk. Kigwangala.
Alipendekeza kwamba bima ni lazima itoe huduma muhimu za afya ikiwa ni pamoja na kinga, matibabu na huduma za dharura, ambazo zinapaswa kuwa za ubora wa juu.
Alisema mfumo wa bima ya afya Tanzania, unapaswa kulinda watu dhidi ya mzigo wa gharama kubwa za matibabu na kwamba chanzo cha fedha kinapaswa kuwa endelevu katika tozo za bima, michango ya serikali na vyanzo vingine vya fedha.
Alipendekeza kwamba, mfumo wa utozaji wa tozo unapaswa kuwa wa haki, wenye kipato kikubwa wanachangia zaidi ili kusaidia makundi yenye kipato cha chini.
Kadhalika, alipendekeza kanuni za bima ya afya kwa wote za mwaka 2024 zirekebishwe ili kuweka wazi vyanzo vya fedha kwa ajili ya watu wasio na uwezo, namna ya kuwatambua wasio na uwezo na namna ya kuusimamia mfuko wa watu wa kundi hilo.
Dk. Kigwangala ametoa mapendekezo hayo kutokana na agizo la Rais wa Marekani Donald Trump la kusitisha misaada ya usambazaji wa dawa za Virusi vya Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria (PEPFAR) na miradi mingine.
Taarifa iliyotolewa na USAID ilieleza kuwa kuanzia Ijumaa saa 11: 59 jioni, wafanyakazi wote wa USAID walioajiriwa moja kwa moja duniani watapewa likizo ya usimamizi, na kwamba wafanyakazi waliotenguliwa kushughulikia majukumu muhimu ya shirika, uongozi mkuu, na programu maalum wataendelea na kazi kama kawaida.
Ilieleza kuwa wafanyakazi walioteuliwa kuendelea na kazi watapewa taarifa rasmi kutoka kwa uongozi wa Shirika, Februari 6, mwaka huu saa 3:00 usiku.
Aidha, wafanyakazi walio nje ya Marekani, Shirika kwa kushirikiana na Idara ya Mambo ya Nje ya Marekani, inajipanga kuwarejesha nchini humo ndani ya siku 30, kulingana na taratibu za sheria husika.
USAID imetangaza kusitisha baadhi ya mikataba ya Huduma za Kibinafsi (PSCs) na Mikataba ya Huduma ya Ushirika (ISCs) ambayo haijatajwa kuwa ya msingi.
Jana wabunge Democratic nchini Marekani wameandamana wakisema uamuzi huo ni kinyume na uamuzi wa kumteua Mfanyabiashara Elon Musk kuwa Mkuu wa Kitengo cha Ufanisi wa Serikali si sawa kwa kuwa hana mamlaka ya kufungwa kwa shirika hilo.
Mbunge Gerry Connolly akizungumza kwenye maandamano hayo, alisema hakuna mtu yeyote anayeweza kuvunja shirika hilo, bali ni Bunge pekee lenye nguvu hiyo.
Hata hivyo, Trump amemtetea Musk kuwa hawezi kufanya chochote bila idhini ya Ikulu na hatua ya kuvunjwa kwa shirika hilo amepewa baraka na serikali.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED