MWAKA 2008 Edward Lowassa wakati huo akiwa Waziri Mkuu, alijiuzulu nafasi hiyo kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kashfa ya kutuhumiwa kuhusika kuibeba kampuni ya Richmond, ambayo licha ya kupewa jukumu la kuzalisha umeme, haikufanya hivyo na nchi ikazidi kubaki gizani.
Mwanasiasa huyo alijua umuhimu wa kutotengeneza maadui, badala yake alijitahidi kuwafanya marafiki wale katika siasa walikuwa wakimchukia na kuwaacha wamkosoe au wamseme watakavyo.
Wakati akitangaza kujiuzulu, alilalamika kutopewa nafasi ya kujieleza kuhusu tuhuma hizo, na kuhitimisha kuwa shida ni huu uwaziri mkuu, hivyo akaamua kuacha nafasi hiyo.
Baada ya uamuzi wake huo, baadhi ya wanasiasa wakiwamo wa kutoka CCM na upinzani, walimpachika kila aina ya majina ya kashfa na kurushiwa maneno mengi kuhusu tuhuma hizo, hata Richmond ikitafsiriwa kuwa ni kampuni yake binafsi iitwayo ‘Rich Monduli.’
Lakini mwenyewe hakuthubutu kufungua mdomo wake kuwajibu au kulumbana nao, badala yake alikaa kimya na kuendelea na shughuli zake zikiwamo za kisiasa wakati huo akiwa mbunge wa Monduli.
Lowassa ambaye sasa ni marehemu, mwaka 2015 alikuwa miongoni msururu mrefu wa makada wa CCM walioomba ridhaa ya chama hicho, kumpitisha kuwania urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka huo.
Hata hivyo, alihama chama hicho na kwenda CHADEMA dakika za mwisho, baada ya kuona amekatwa katika mchakato wa kumpata mgombea wa chama hicho wa kuchuana na wapinzani.
Kuondoka kwake ilikuwa ni kama kufungulia upya matusi, kejeli, kashfa na kila neno baya dhidi yake kutoka kwa baadhi ya makada wa CCM, lakini kama kawaida yake hakufungua mdomo kuwajibu.
Badala yake aliendelea na kampeni za kuwania urais kupitia chama kipya alichohamia na kuleta ushindani mkali katika kampeni za uchaguzi kwenye mikoa mbalimbali alikokuwa akipita.
Huku kila aina ya vijembe na kejeli na mambo mengine vikiendelea dhidi yake katika kampeni hizo, Lowassa aliendelea kumwaga sera za chama kipya na mikakati yake ya ambavyo angeongoza nchi.
Baadaye mwanasiasa huyo alirudi CCM hadi alipopatwa na mauti, lakini kama alivyohama CCM kwenda upinzani, ndivyo pia alirudi CCM bila kuthubutu kupanua mdomo wake kutukana na kukashifu kule alikotoka.
Tangu aliporudi CCM, aliendelea kuwa kimya. Huyo ndiye Lowassa mwenyewe ambaye alikuwa na uwezo wa kuvumilia siasa za majitaka alizokumbana nazo akiwa CCM na hata nje ya chama hicho.
Ninadhani yapo mengi ambayo wanasiasa wanaweza kujifunza kwake kupitia uvumilivu wake licha ya kutukanwa kiasi kile,lakini hakuthubutu kujibu neno au kuanzisha malumbano, badala yake alinyamaza kimya.
Mwanasiasa huyo alijua umuhimu wa kutotengeneza maadui, badala yake alijitahidi kuwafanya marafiki wale katika siasa walikuwa wakimchukia na kuwaacha wamkosoe au wamseme watakavyo.
Alikubali kukosolewa, kusemwa vibaya hata kwa yale ambayo hakutenda. Mfumo wake huo wa maisha katika siasa za Tanzania, atakuwa ameawachia wanasiasa jambo la kujifunza kuvumiliana.
Huyo ndiye Lowassa ambaye alikuwa tayari kusemwa vibaya, lakini pia kukosolewa, kwani alitambua kwamba kukosolewa ni jambo la kawaida ambalo linampa mtu nafasi ya kujisahihisha pale alipokosea.
Lowassa ametangulia, lakini amewaachia wanasiasa somo la uvumulivu wa kisiasa, kwamba wanaweza kutofautiana,lakini wakavumiliana kwa kuwa wote wanajenga nyumba moja ambayo ni Tanzania.
Mwili wake unatarajiwa kuagwa leo kwenye ibada itakayofanyika katika Kanisa la Azania Front jijini Dar es Salaam, kisha kesho utasafirishwa kwenda jijini Arusha na kuagwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na familia ya Lowassa, siku ya Ijumaa ibada ya kuaga mwili wake itafanyika Monduli na kufuatiwa na maziko yatakayofanyika Monduli Jumamosi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED