Tatizo la mafao kwa wastaafu lipatiwe ufumbuzi wa kudumu

Nipashe
Published at 11:44 AM Jan 30 2025
Tatizo la mafao kwa wastaafu lipatiwe ufumbuzi wa kudumu.
Picha: Mtandao
Tatizo la mafao kwa wastaafu lipatiwe ufumbuzi wa kudumu.

KWA muda mrefu kumekuwa na kilio kuhusu kucheleweshwa kwa malipo ya wastaafu kwa sababu mbalimbali. Miongoni mwa sababu hizo ni kutokuwapo kwa taarifa zao Hazina au kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii ambazo zinapaswa kuwasilishwa na waajiri kabla ya mfanyakazi kufikia ukomo wa ajira yake.

Mifuko hiyo, ambayo hulipa mafao ya watumishi wa umma na wale wa sekta binafsi pamoja na Hazina ambako hulipwa mafao ya wastaafu kama vile kwenye vyombo vya ulinzi na usalama, pia imekuwa ikichelewesha malipo hayo ama kwa sababu waajiri hushindwa kuwasilisha makato ya kila mwezi ya wafanyakazi au kushindwa kupeleka taarifa za wafanyakazi ili uandaaji malipo kabla ya kustaafu ufanyike.

Kutokana na kuwapo kwa changamoto hiyo, baadhi ya watumishi wamekuwa wakihangaika kufuatilia mafao yao na wakati mwingine kukata tamaa na hata kufariki dunia kabla ya kuyafaidi licha ya kutumia nguvu zao nyingi katika kufanya kazi. Pia hali hiyo imewafanya baadhi ya watumishi walioko bado kwenye ajira kuona kama vile kustaafu ni adhabu.

Mfano wa watu ambao wamefanya kazi na kuanza kuhangaika kufuatilia mafao ni askari wastaafu wa Jeshi la Polisi ambao juzi wakati wa kipindi cha Maswali na Majibu Bungeni, mbunge mmoja alihoji ni kiasi gani ambacho wastaafu hao wa chombo kilichopewa dhamana ya kusimamia usalama wa raia na mali zao.

Katika majibu ya serikali ilielezwa kuwa wastaafu hao wanadai mafao ya zaidi ya Sh. bilioni 97.1 na kwamba kati ya hizo, Sh. bilioni 75.2 zmepelekwa Hazina kwa ajili ya malipo baada ya kufanyika kwa uhakiki wa wastaafu hao. Pia serikali ilisema mafao ya takribani Sh. bilioni 21.9 bado yanahakikiwa kabla ya watumishi hao kulipwa.

Tatizo kubwa, kwa mtazamo yakinifu, linaloonekana hapa ni uhakikiwa wa wastaafu hao baada ya kumaliza utumishi wao wa jambo ambalo lilipaswa kufanyika miezi au hata mwaka kabla ya kufikia muda wa kuondoka kwenye ajira. Badala ya kufanya hivyo, kazi hiyo ya uhakiki imekuwa ikifanyika baada ya mtu kutoka katika utumishi jambo ambalo husababisha usumbufu mkubwa kwa wahusika. 

Chanzo kikubwa cha kuwapo kwa changamoto hiyo ni majina na taarifa za wahusika kutokuwa katika mfumo na matokeo yake mtu anaanza kuhakikiwa upya baada ya kustaafu. Inakuwaje mtu aanze kuhakikiwa baada ya kustaafu wa kuulizwa mwaka aliozaliwa, lini alipandishwa cheo na kama anadaiwa na taasisi yoyote ya fedha iwapo aliwahi kukopa na hajamaliza deni kabla ya kustaafu.

Kuwapo kwa hali hiyo pia hutengeneza mazingira ya rushwa kwa baadhi ya watumishi wa Hazina na mifuko kutaka wastaafu hao kutoa chochote ili wasizungushwe na milolongo ya kufuatilia mafao. Kwa kuepuka usumbufu huo, baadhi ya wahusika wamekuwa wakaingia katika mtego huo kwa sababu ya kukataa kuchoshwa na hadithi ya ‘njoo kesho, njoo kesho’.

Suala la mafao kwa wastaafu kwa sasa limekuwa sawa na hadithi isiyokuwa na mwisho. Ni vyema sasa serikali ikachukua hatua madhubuti ili kukomesha suala hili na kurejesha furaha kwa wastaafu ambao kwa sasa wanaona kufikia hatua hiyo ni kama mwisho wa maisha yao.

Waajiri wote, zikiwamo taasisi za serikali, wanapaswa kupeleka taarifa za wafanyakazi ambao wamebakiza muda mfupi kustaafu ili waandaliwe mafao yao na hatimaye kuyapata baada ya kuondoka katika utumishi.

Pia, kama kuna uwezekano, sheria inayohusu mifuko ya jamii, pensheni na mafao kwa wastaafu ifanyiwe marekebisho ikiwamo kuweka kipengele cha adhabu kwa mwajiri ambaye atachelewesha kupeleka taarifa za mtumishi kabla ya kustaafu.