Wasichana, wanawake hawa wasaidiwe na wataalamu, kabla hawajapotea

By Joyce Lameck , Nipashe
Published at 08:56 AM Jan 24 2025
Ugonjwa wa akili.
Picha:Mtandao
Ugonjwa wa akili.

BAADHI ya watu wanafikiri kwamba utoaji mimba daima ni makosa. Pia, kuna wengine wanaodhani kwamba kutoa mimba ni sawa, ilhali maisha ya mama yanakuwa hatarini.

Pia kuna wengine wanaofikiri kwamba, kuna hali mbalimbali, ambazo kutoa mimba kunakubalika kimaadili.

Niseme kuwa siku zote, utoaji mimba usio salama, hauishii kuathiri afya pekee, hata kiakili. Kwa ujumla, inaishia kusababisha madhara kwa mama aliyetoa mimba, pasipo kuzingatia picha pana ya usalama wake, ikiwamo njia zisizo salama kwa kuogopa sheria, pamoja na adhabu iliyopo nchini.

Mtaalamu wa saikolojia kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, ambaye ni mtaalamu wa kutibu magonjwa ya akili, Dk. Faithness Kiondo, ana orodha ya madhara ambayo mama anayapata kiakili, pale anapotumia njia zisizo salama kutoa mimba.

Anaeleza kwamba, wanawake wengi hupatwa changamoto ya maradhi sonona, yanayotokana na msongo wa mawazo, pia upweke kifikra bila kupata suluhu ya kile anachokifikiri kila wakati.

Vilevile anasema, kuna wakati mama aliyetoa mimba kwa njia ambazo si salama, anaweza kupata hali ya kiwewe ambalo ni tatizo la kiakili lililosababishwa na wasiwasi, mhemko kama zao la tukio hilo.

Dk. Faithness anafafanua kuwa mwanamke, msichana anakuwa ni wa kuona aibu na kujiona ana hatia kila wakati, pindi anapotafakari kuhusu tukio la utoaji mimba usio salama kwani njia alizotumia hazikuwa salama na mafichoni.

Mbali na changamoto hizo, mwanasaikolojia huyo anasema kuwa, mama huyo anaishia kutumia kilevi, akiamini itamsaidia kuwa sawa kiakili, lakini kumbe inamuongezea matatizo si kiafya pekee, bali hata kiakili.

Mtaalamu huyo anaeleza kuwa mama aliyekutana na changamoto hiyo, anaweza kuchukua hatua mbaya zaidi ya kujaribu au kutaka kujiua, kutokana na msongo wa mawazo yaliyosababishwa na utoaji mimba usio salama.

Vilevile waathirika wa utoaji mimba usio salama wanakabiliwa na matatizo ya muda mrefu kama utasa na maumivu ya tumbo, hata kuharibika kwa kizazi na kubwa zaidi ni kupoteza maisha kwa mama na mtoto aliyekuwa tumboni.

Madhara hayo hutokea pale zinapotumika njia zisizo salama kutoa mimba, kwani mara nyingi hata mtoa huduma si yule mwenye elimu sahihi na kutokuwa na weledi au ufanisi wa kazi yake, hivyo hufanya bila kujali madhara ya kiakili kwa mama.

Hata hivyo, mtazamo hasi wa jamii kwa kinamama wanatoa mimba, ndio unaosababisha kuchukua uamuzi inayowapeleka kutumia njia zisizokuwa salama katika kutoa mimba na kusababisha madhara kiafya na hata kiakili.

Hata hivyo, kutokuwapo kwa elimu na uhamasishaji wa kutosha wa afya ya uzazi makundi mbalimbali na hasa vijana na wanaume kumesababisha kuongezeka kwa magonjwa ya ngono, pamoja na matatizo ya mimba zisizotarajiwa, hasa maeneo ya vijijini.

Pia, mila potofu zimechangia katika kuzorotesha afya ya uzazi katika baadhi ya maeneo nchini, hasa kwa yale ambayo bado hayajafikiwa na elimu, huduma kuhusu uzazi salama kwa mama na mtoto.

Wanawake wanaohitaji kutoa mimba wako kinyume na maadili ya kitamaduni ambayo yanajumuisha wazo kwamba ngono inatumika tu, kwa uzazi na kwamba wanapaswa kubaki safi kingono mpaka pale watakapo hitaji uzazi.

Serikali nayo kupitia Wizara ya Afya katika mapambano dhidi ya changamoto ya utoaji mimba usio salama, ikiwamo kutoa elimu juu ya afya ya uzazi kwa watoto wa kike ambao wapo chini ya umri wa kuzaa

Vilevile wizara kupitia vitengo vyake, imeendelea kutoa elimu kwa klabu za vijana na vijana balehe kutojihusisha na ngono zembe, ili kuepuka kupata mimba zisizotarajiwa ambazo hupelekea kuongezeka vitendo vya utoaji mimba usio salama.

Pia, inaendelea kusimamia utoaji wa huduma za uzazi wa mpango katika vituo vya huduma bila malipo, ili kuwawezesha wanawake na wanaume kuzuia mimba zisizotarajiwa.

Hata hivyo wajawazito kuhudhuria katika kliniki za uzazi wa mpango itawasaidia, waweze kupatiwa elimu ya afya ya uzazi ikiwamo jinsi ya kuepukana na mimba zisizotarajiwa, hata kuondokana na uavyaji wa mimba usio salama.