Kufungiwa Simba iwe fundisho

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 08:18 AM Jan 18 2025
Mshabiki wa Simba.
Picha: Mtandao
Mshabiki wa Simba.

WAKATI mwingine kwenye maisha si lazima kulipiza kisasi. Na mara nyingi anayelipiza kisasi huonekana kuwa ndiye mwenye matatizo. Unaweza ukaonewa au kufanyiwa kibaya watu wasione, lakini ukiamua kurudisha au kulipiza kisasi kila mmoja atakushukia kuwa umetenda ndivyo sivyo.

Hata wale waliopo magerezani kwa sasa wamefungwa, baadhi yao wamefanya hivyo kwa kulipiza kisasi. Kwa maana hiyo tunajifunza kuwa makini sana na kitu cha kurudishia, au kulipa kisasi.

Hiki ndicho kilichowakuta mashabiki wa Simba. Baada ya kuchokozwa kidogo tu na mashabiki wachache wa CS Sfaxien, wakaamua kuwarudishia. Kibaya zaidi ni kwamba wao walikuwa wengi dhidi ya mashabiki wachache wakorofi ambao hawakuwa na uwezo wa kujitetea kwa chochote pale walipofanyiwa vurugu.

Nasema Simba ilifanyiwa vurugu nikirejea taarifa rasmi ya Jeshi la Polisi iliyotolewa, Desemba 15 mwaka jana baada ya kumalizika kwa mchezo huo.

Taarifa hiyo iliyotolewa na Kamanda Kanda Maalum ya Polisi, (SACP) Jumanne Muliro, ilibainisha kuwa kulitokea fujo kwenye mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa baada ya kumalizika kwa mchezo kati ya Simba dhidi ya CS Sfaxien.

"Fujo hizo zilisababishwa na mashabiki wa timu ya CS Sfaxien kutoridhika na maamuzi ya refa wa mchezo huo kuchezesha mechi kwa dakika zaidi ya saba ambazo zliziongezwa kama dakika za kufidia zile zilizopotea jambo ambalo lilisababisha Simba kupata bao la pili na la ushindi. 

Wachezaji ndani ya uwanja na benchi la ufundi la timu hiyo walikasirika, wakaamua kumfuata mwamuzi wa mchezo na kuanza kufanya vitendo vya kumshambulia.

Katika fujo hizo, shabiki mmoja wa CS Sfaxien aliumia na kupatiwa huduma ya kwanza, akaruhusiwa, huku viti vya rangi ya bluu 156 viking'olewa na mashabiki pamoja na vya rangi ya mchungwa 100," ilisema sehemu ya taarifa hiyo ya Polisi.

Hii ni taarifa iliyojitosheleza kabisa kwani imeainisha kila kitu mpaka sababu. Kwa maana hiyo baada ya kuchokozwa mashabiki wa Simba walishindwa kuzuia hasira zao, badala yake sasa wamefungiwa kuingia uwanjani katika mechi ya kesho dhidi ya CS Constantine.

Awali mashabiki wa Simba walipanga kujazana uwanjani kwani kwao si mechi ambayo ilikuwa ya presha sana kwa sababu tayari wameshatinga robo fainali. 

Kwao ilionekana ni ya kwenda 'kuinjoi' zaidi, kwa sasa hali sivyo ilivyo tena. Watalazimika kubaki majumbani, kwenye vipanda umiza na wengine wameambiwa waende Temeke Mwembeyanga ambako kutafungwa TV kubwa.

Ni nadra sana kuona timu za Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, Kusini na hata Magharibi zikifungiwa. Mara nyingi timu zinazopewa adhabu hizi ni za Afrika Kaskazini. 

Timu karibuni zote kubwa za Afrika Kaskazini zimeshakutana na kadhia hii, wenyewe ni kama wamezoea na ndiyo sehemu ya maisha yao, lakini siyo huku. 

Mashabiki wa Simba wameonekana kuhuzunika na adhabu hii, hili lisiwe fundisho kwa mashabiki si wa Simba tu, bali wa timu zote za Tanzania ambazo timu zao zitafuzu kucheza michezo ya kimataifa msimu ujao.

Mashabiki wajifunze 'fair play' na uvumilivu wakiwa uwanjani, na kuepuka kukubali kuchokozeka kirahisi na wapinzani hasa mashabiki wa Afrika Kaskazini ambao wao kufanya fujo na kufungiwa ni kama sehemu tu ya utamaduni.

Mfano, sikuona sababu ya mashabiki wa Simba kuwa na hasira kiasi kile kwani tayari timu yao ilikuwa imepata bao la pili, badala yake wangekuwa wanashangilia zaidi kuliko kupigana na wageni wao.

Nadhani baada ya hili kutokea, mashabiki wote Bongo watakuwa wamejifunza na hawatorudia tena kwani CAF hawangalii mtu usoni, wala kuionea aibu klabu kwa sababu ni kubwa au ndogo, kwani sheria na kanuni ni kama msumeno, unakata huku na huku.