Serikali inastahili pongezi bwawa la Kidunda, kasi zaidi inahitajika

Nipashe
Published at 10:04 AM Feb 09 2025
Bwawa la Kidunda
Picha: Mtandao
Bwawa la Kidunda

SERIKALI kupitia Wizara ya Maji kwa kushirikiana na Mamlaka za majisafi na Usafi wa Mazingira imekuwa ikifanya kila jitihada kuhakikisha wananchi katika maeneo mbalimbali ya nchi wanapata huduma ya maji safi na salama.

Katika kusisitiza hiyo, serikali ya awamu ya sita imeibuka na kaulimbiu ya kumtua mama ndoo kichwani. 

Kaulimbiu hiyo iliyobuniwa na Rais Samia Suhulu Hassan, inatokana na ukweli kwamba mwanamke ndiye mhusika mkuu katika suala zima la kuhakikisha maji yanapatikana katika familia kwa ajili ya matumizi mbalimbali. 

Kutokana na upungufu wa maji katika maeneo mbalimbali, wanawake huamka mapema alfajiri kwa ajili ya kutafuta maji ambayo hupatikana kwa umbali mrefu. 

Wakati wa harakati za kusaka huduma hiyo, wanawake wamekuwa wakitoa simulizi mbalimbali kuhusu majanga yanayowakabili kama baadhi yao kupoteza maisha kwa kushambuliwa na wanyama wakali na wengine kufanyiwa vitendo vya kinyama kama vile kubakwa. 

Baadhi yao pia wamekuwa wakidai kuwa ndoa zao ziko hatarini kuvunjika kwa kuwa wamekuwa wakitumia muda mwingi kutafuta maji huku wenza wao wakidhani kwamba wanakuwa na uhusiano na wanaume wengine.

Hiyo  ndiyo hali halisi ndiyo maana Rais Samia aliamua kuibuka na kauli hiyo ili kuwaokoa wanawake na madhila yanayowakumba. 

Kwa ujumla, hali hiyo pia imesababisha wanawake kutumia muda mwingi kutafuta maji badala ya kufanya shughuli za uzalishaji. Kimsingi, mwanamke anabeba dhima kubwa katika familia kwa kuwa ndiyo mhimili mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa familia, jamii na taifa kwa ujumla.

Dar es Salaam ni moja ya maeneo yanayokumbwa na shida ya maji mara kwa mara hatua ambayo imeifanya serikali kuelekeza nguvu nyingi kuhakikisha huduma hiyo inapatikana. Katika kufanya hivyo, Mamlaka ya  Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali zikiwamo uchimbaji wa visima virefu katika sehemu mbalimbali kama Kigamboni. 

Hatua hiyo ni moja ya juhudi za kuongeza upatikanaji wa huduma na kuepuka utegemezi wa mitambo ya Ruvu Juu na Ruvu Chini ambayo uzalishaji wake unatokana na maji kutoka mto Ruvu ambao wakati mwingine hupungua kina nyakati za kiangazi.

Hivi karibuni, mamlaka hiyo ilialika wadau mbalimbali kwenda kushuhudia maendeleo ya ujenzi wa Mradi wa Bwawa la Kidunda, lililoko Morogoro ambalo baada ya kukamilika kwake, linatarajiwa kuhifadhi lita bilioni 190.

Kukamilika kwa mradi huo ambao umekuwa katika mipango ya maendeleo tangu Tanzania ilipopata Uhuru mwaka 1961, unatekelezwa kwa pesa za ndani na utapunguza kwa kiasi kikubwa upungufu wa maji mkoani Dar es Salaam, Morogoro  na baadhi ya maeneo ya mkoa wa Pwani ambayo yanahudumiwa na DAWASA. Kwa sasa utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 27.

Kwa mujibu wa taarifa ya DAWASA, mradi huo unatarajiwa kugharimu zaidi ya Sh. bilioni 336 hadi kukamilika kwake unalenga kuhakikisha upatikanaji wa maji wa uhakika kwa wakazi wa mikoa hiyo ifikapo Desemba 2026 utakapokamilika sambamba na kutoa maji ya uhakika, mradi huo unatarajiwa kuwa suluhisho la muda mrefu kwa uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika mikoa inayonufaika.

Kwa utekelezaji huo, serikali inastahili pongezi za dhati kwa kuwa imeonesha kwa vitendo kwamba ina dhamira ya kweli katika kuhakikisha wananchi wake wanaondokana na adha ya kukosa huduma hiyo ambayo imekuwapo kwa muda mrefu. 

Pamoja na pongezi hizo, ahadi ya kwamba mradi huo utakamilika katika muda uliopangwa inapaswa kutekelezwa ili kuwapa kicheko wananchi ya kupata maji kwa uhakika badala ya hali ilivyo sasa ambapo kuna tatizo la upatikanaji wa huduma hiyo.