CCM Kilimanjaro yamfukuza uanachama Dk. Godfrey Malisa

By Mary Mosha , Nipashe
Published at 04:20 PM Feb 10 2025
Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Mercy Malisa.

Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kilimanjaro kimemfukuza uanachama Dk. Godfrey Malisa kufuatia matamko yake yanayosambaa kwenye mitandao ya kijamii dhidi ya Mwenyekiti wa CCM Taifa ambaye pia ni Rais wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza kuhusu uamuzi huo, Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Mercy Malisa, amesema hatua hiyo imefikiwa baada ya Dk. Malisa kupuuza maonyo ya muda mrefu aliyopewa na chama.

"Kwa mujibu wa taratibu za chama, mwanachama huyo amefukuzwa kwa kukosa sifa za kuendelea kuwa mwanachama wa CCM baada ya kubeza maamuzi halali yaliyofanywa na Mkutano Mkuu wa CCM Taifa uliofanyika Februari 19, jijini Dodoma," amesema Mercy.

Ameongeza kuwa baada ya mkutano huo, Dk. Malisa alianza kutoa matamko yanayovuruga umoja na mshikamano wa chama na Taifa kwa ujumla, huku akidai kuwa mkutano huo ulivunja Katiba ya CCM.

"Sisi, ambao tulikuwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa na kushiriki mchakato wa kumpata mgombea wa chama, tunathibitisha bila shaka yoyote kwamba hakuna kipengele chochote cha Katiba ya CCM kilichovunjwa," amesisitiza Mercy.

Kwa mujibu wa kanuni za maadili ya CCM, kifungu cha 6(3)(b), "Mwanachama au kiongozi yeyote anayekataa maamuzi ya kikao halali cha chama atakuwa ametenda kosa la utovu wa nidhamu na ataadhibiwa kwa mujibu wa kanuni hizi."

Aidha, kifungu cha 6(3)(c) kinasema: "Mwanachama atakayekataa kumuunga mkono mgombea wa CCM aliyeteuliwa na kikao halali cha chama, na badala yake akafanya kampeni za siri au za wazi dhidi yake, atakuwa ametenda kosa la usaliti na anastahili kufukuzwa uanachama."

Vilevile, Katiba ya CCM, Ibara ya 89(4), inaeleza kuwa miongoni mwa kazi za Halmashauri Kuu ya Mkoa, kama ilivyoainishwa katika kifungu cha 14, ni "kumwachisha au kumfukuza uanachama mwanachama yeyote endapo tabia na mwenendo wake vinamuondolea sifa za uanachama."

Mercy amesisitiza kuwa kikao cha Halmashauri Kuu ya Mkoa kimetimiza matakwa ya kikatiba kwa kumfukuza Dk. Malisa kutokana na kukaidi maamuzi halali ya chama.

"Mkutano Mkuu wa CCM ndio kikao cha juu kabisa ndani ya chama, na hakuna mwanachama anayepaswa kupinga maamuzi yake. Kwa kuwa Dk. Malisa ameendelea kukaidi na kuvunja matakwa ya chama, tunatangaza rasmi kuwa kuanzia leo si mwanachama wa CCM tena," amehitimisha Mercy.