PSSSF yatoa elimu kwa wajumbe wa baraza la wafanyakazi NIDA

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:43 PM Feb 10 2025
PSSSF yatoa elimu kwa wajumbe wa baraza la wafanyakazi NIDA.
Picha: Mpigapicha Wetu
PSSSF yatoa elimu kwa wajumbe wa baraza la wafanyakazi NIDA.

MFUKO wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), umetoa elimu ya Hifadhi ya Jamii na shughuli zinazotekelezwa na mfuko huo kwa wajumbe wa baraza la Wafanyakazi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) jijini Arusha, leo Februari 10, 2025.

Akitoa wasilisho la utekelezaji wa majukumu ya mfuko huo mbele ya wajumbe hao wapatao 100 wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), James Kaji, Afisa Mwandamizi wa PSSSF, Kanda ya Kaskazini, Venance Mwaijibe, akiwa amefuatana na Meneja wa Kanda hiyo, Linda Balati, amesema PSSSF imeboresha utoaji wa huduma zake ili kuendana na mabadiliko ya teknolojia lakini pia malengo ya serikali yanayotaka mifumo ya serikali kusomana ili kurahisisha utoaji wa huduma, ambapo kwa sasa Mwanachama wa PSSSF anapata huduma zote kupitia mtandao maarufu PSSSF Kidijitali.

Mwaijibe, ametaja miongoni mwa huduma ambazo mwanachama anazoweza kuzipata kupitia mtandao ni pamoja na taarifa za michango yake, taarifa za uwekezaji, lakini pia namna ya kuwasilisha madai mbalimbali.

“Huduma ya PSSSF kidijitali inamuwezesha mwanachama kujihudumia mwenyewe kupitia simu janja, kishikwambi (tablet) au computer; Huduma hii pia inamuwezesha mwanachama anayekaribia kustaafu, kuweza kuwasilisha madai kupitia mtandao.” amesisitiza.

Aidha Afisa Mafao Mkuu wa PSSSF Kanda ya Kaskazini, Baraka Kitundu, amesema, mfuko umeanza kutekeleza maagizo ya serikali ya kuanza kulipa Mafao kwa kutumia utaratibu wa kikokotoo kilichoboreshwa na tayari kuanzia Januari mwaka huu wa 2025, pensheni ya kila mwezi imeongezeka kwa asilimia 2.

Amesema, katika maboresho hayo, mstaafu yeyote anayepokea pensheni katika Mfuko wa PSSSF akifariki, Mfuko utatoa kiasi cha Sh 500,000.00 kwa ajili ya maziko (funeral grant), huku Mstaafu yoyote akifariki wategemezi wake wanaotambuliwa na sheria ya Mfuko watalipwa mkupuo wa miezi 36 wa pensheni ya mwezi ya mstaafu husika, amefafanua Kitundu.