Waliyozungumza CHADEMA, Jaji Warioba haya hapa

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:18 PM Feb 10 2025
Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Tundu Lissu Waziri Mkuu Mstaafu na Jaji Joseph Warioba (katikati)
Picha: Mtandao
Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Tundu Lissu Waziri Mkuu Mstaafu na Jaji Joseph Warioba (katikati)

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, kimeweka bayana kiini cha mazungumzo yake na Waziri Mkuu Mstaafu Jaji Joseph Warioba ofisini kwake leo jijini Dar es Salaa.

Mambo hayo ni kuhusu uchaguzi wa ndani ya chama uliomalizika hivi karibuni na pia kuhusu hali halisi kuhusiana na uchaguzi uliomalizika wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji wa mwaka 2024 na ulazima wa kuwa na mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi Tanzania ili kuwa na chaguzi zinazoaminika na zisizo na dosari.

Kwa mujibu wa taraifa iliyotolewa leo, Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Tundu Lissu akiwa ameambatana na Naibu Katibu Mkuu Bara, Amani Golugwa walimtembelea kiongozi huyo ofisini kwake.

Uchaguzi wa CHADEMA ulifanyika Januari 21, mwaka huu, na Lissu aliibuka mshindi huku aliyekuwa Mwenyekiti wa miaka 21, Freeman Mbowe akiangishwa.

Pia chama hicho kimetangaza msimamo kuwa hakitakwenda kwenye uchaguzi mkuu kama hakutakuwa na mabadiliko kwenye mifumo ya uchaguzi na kuwa na mazingira ya haki kwa wadau wote.

Aidha, kililalamikia uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Novemba 27,2024 kwa wagombea wake wengi kukatwa, watu wawili kufariki dunia na wengine kadhaa kujeruhiwa.