Zaidi ya wakazi 500,000 wa visiwa vya Ziwa Victoria wamenufaika na huduma za afya zinazotolewa na meli ya matibabu MV Jubilee Hope, inayoendeshwa na Kanisa la Afrika Inland Church Tanzania (AICT) Dayosisi ya Geita, kwa kushirikiana na shirika la Vine Trust kutoka Scotland na Kampuni ya Geita Gold Mine (GGML).
Katika maadhimisho ya miaka 10 ya huduma ya MV Jubilee Hope na uzinduzi wa meli mpya MV Lady Jean, Mkurugenzi wa mradi, Mchungaji Samweli Limbe, alisema meli hiyo imetoa huduma za afya katika visiwa vya mkoa wa Kagera, vikiwemo Ikuza, Chakazibwe, Mazinga, Bumbile, Kelebe, Goziba, Butwa, Isimajeli, Juma na Nyamango.
Limbe alieleza kuwa mafanikio haya yamewezekana kwa ushirikiano wa GGML, ambayo inagharamia mafuta, matengenezo na vilainishi vya meli, huku Vine Trust likitoa fedha kwa ajili ya uendeshaji. Pia, alisema bila ushirikiano wa serikali, huduma hiyo isingefanikiwa.
Mwenyekiti wa Vine Trust na daktari wa kujitolea, Dk. Claire Bawn, alisema mchakato wa kununua meli hiyo ulianza mwaka 2012 wakati wa maadhimisho ya Jubilee ya miaka 60 ya uongozi wa Malkia Elizabeth, na kufanikishwa mwaka 2014. “Nina furaha kuona zaidi ya watu nusu milioni wakinufaika na huduma hii, na tuko tayari kuendelea kushirikiana kwa miaka mingi zaidi,” alisema.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa GGML, Simon Shayo, alisema wanajivunia kuwa sehemu ya mradi huu, ambao umeleta mapinduzi katika maisha ya jamii za visiwani. Alisisitiza kuwa huduma ya afya visiwani ni changamoto, hasa kwa dharura kama wanawake wanaohitaji kujifungua usiku.
"Tunaishukuru serikali kwa kutambua umuhimu wa huduma hii. GGML itaendelea kushirikiana na wadau katika sekta za afya, elimu na miundombinu, ambapo kila mwaka tunawekeza zaidi ya Sh bilioni 9 wilayani Geita,” alisema Shayo. Pia, alitangaza kuwa GGML imeongeza ufadhili wa mradi huu kutoka Dola 120,000 hadi Dola 240,000 kwa mwaka.
Mkurugenzi wa Usalama, Ulinzi na Utunzaji Mazingira wa Tasac, Leticia Mtaki, alisema meli hiyo ina urefu wa mita 23.7 na upana wa mita 6.4, ikiwa na wahudumu wa afya 15 na mabaharia 8. Alisema wamehakikisha usalama wa chombo hicho kwa miaka 10 bila changamoto yoyote kubwa.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, aliwashukuru wadau kwa kusaidia sekta ya afya visiwani, akisema kuwa huduma hiyo imepunguza magonjwa na kuboresha ustawi wa jamii. “Tumeona mabadiliko makubwa katika afya ya uzazi, matibabu ya malaria, utoaji wa chanjo, na upasuaji mdogo wa kinywa na meno,” alisema Mtanda.
Aliongeza kuwa ujio wa MV Lady Jean utaimarisha huduma za afya na kuboresha utoaji wa huduma za dharura kwa haraka na ufanisi zaidi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED