TAMA yanoa wakunga wa Dar

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 07:58 PM Feb 10 2025
Mkunga mkufunzi, Elizabeth Mwakalinga kutoka Chuo cha Uuguzi na Ukunga Bagamoyo Pwani, akigawa karatasi za mtihani kwa wakunga, katika mafunzo hayo.
Picha: Sabato Kasika
Mkunga mkufunzi, Elizabeth Mwakalinga kutoka Chuo cha Uuguzi na Ukunga Bagamoyo Pwani, akigawa karatasi za mtihani kwa wakunga, katika mafunzo hayo.

WAKUNGA wamekumbushwa kushiriki mafunzo kila mara wanapopata nafasi, ili waweze kujiongezea maarifa ya kuwawezesha kufanya kazi yao kwa ufanisi.

Wito huo umetolewa na Rais wa Chama cha Wakunga Tanzania (TAMA), Dk. Beatrice Mwilike jijini Dar es Salaam leo.

Rais huyo alikuwa akizungumza katika mafunzo ya huduma za dharura kwa wakunga kutoka katika zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya, za mkoa na za rufani mkoani Dar es Salaam.

Dk. Beatrice amesema kumekuwapo na changamoto nyingi katika masuala ya uzazi zinazotokana mabadiliko ya tabianchi, na kwamba wakunga wanapaswa wajue jinsi ya kukabiliana nazo.

"Wakati mwingine mzazi anaweza kutokwa na damu nyingi baada ya kujifungua, mwingine anaweza kushindwa kujifungua, hivyo ni muhimu mkunga awe na  mbinu za kusaidia kumaliza tatizo," amesema Dk. Beatrice.

Amefafanua kuwa wapo watoto wanaopoteza maisha siku chache baada ya kuzaliwa, na kwamba kupitia mafunzo mbalimbali ambayo wakunga wanapata, wanaweza kupunguza vifo vya  watoto kwa asilimia 90.

"Mafunzo kazini yana umuhimu mkubwa wa kumsaidia mkunga kufanya kazi yake kwa  usahihi zaidi, kwani anakuwa na uwezo wa kufanikisha utoaji wa huduma bora ambazo zitakuwa na mchango mkubwa wa kutokomeza   vifo vya wajawazito na watoto wachanga," amesema.

Amefafanua kuwa mafunzo hayo ni sehemu mradi wa miaka saba uitwao 'Thamini Uzazi Salama' unaoendeshwa katika mikoa ya Dar es Salaam na Shinyanga.

"TAMA inashirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu Duniani (UNFPA), Tanzania na Chama cha Wakunga cha Canada kuendesha mradi huu na tunatarajia kufikia wakunga 600," amesema.

Mratibu wa Huduma ya Mama na Mtoto mkoa wa Dar es Salaam, Agness Mgaya amesema licha ya kuwapo kwa wito wa kuwataka wanaume kuambatana na wake zao wanapokwenda kujifungua, bado kuna idadi ya wanaume wanaitumia wito huo.

"Tunataka wanaume waambatane na wake zao kwa sababu kuna faida nyingi, ikiwamo elimu kuhusu uzazi Salama, lakini mwitukio bado ni mdogo ni kama asilimia 40 ambao  wanasindikiza wake zao," amesema.

Ameongeza kuwa mjamzito anaweza kuumwa kichwa zikiwa ni dalili za kifafa Cha uzazi, na kwamba mume wake anaweza kumpa Panadol akadhani ni maumivu tu kawaida."

"Lakini anapoambatana na mke wake wakati wa kwenda kliniki au kujifungua, anafundishwa mambo mengi ya kumsaidia kutoa huduma za awali kabla ya kumfikisha katika kituo cha afya," amesema.

Mratibu huyo amesema mkoa wa Dar es Salaam kwa Sasa una vituo 35 vinatoa pia huduma ya upasuaji, na kufafanua kuwa katika mkoa wake wanawake laki moja na hamsini na saba hujifungua kila mwaka.