Jumla ya wanafunzi 11,524 kutoka kaya maskini zilizotambuliwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) wamenufaika na mkopo wa elimu ya juu kwa asilimia 100 ili kuendelea na masomo katika vyuo mbalimbali nchini.
Mkurugenzi wa Mifumo, Tathmini na Mawasiliano wa TASAF, Japhet Boaz, amesema hayo katika maadhimisho ya miaka 20 ya Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) yaliyofanyika leo.
Ameeleza kuwa TASAF na HESLB ziliingia makubaliano ya kushirikiana kwa kuoanisha taarifa zao, kurahisisha utambuzi wa waombaji kutoka kaya maskini, na kuhakikisha wanapata mikopo kwa asilimia 100.
Amesema mpango huu umewezesha wanafunzi kutoka kaya duni kutimiza ndoto zao za elimu ya juu tangu mwaka 2019/2020 hadi 2024/2025. Kwa zaidi ya miaka 10, TASAF imezifikia kaya maskini milioni 1.2 zenye wanakaya zaidi ya milioni 5.2, ambapo watoto 724,867 wanasoma shule za msingi, 341,827 sekondari (O-Level), na 26,308 (A-Level).
Boaz amesisitiza kuwa TASAF inaendelea kusaidia kaya maskini kuongeza kipato, fursa za kiuchumi, na uwezo wa kugharimia mahitaji ya msingi ili kuboresha maisha yao.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED