Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete amesema kwa mwaka 2024/25 imefanya maboresho zaidi kwenye kikokotoo kwa watumishi nchini baada ya mjadala ndani ya Bunge.
Kikwete ameliambia Bunge leo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Mbogwe (CCM), Nicodemas Maganga ambaye amehoji lini serikali itafanya mabadiliko kwenye kikokotoo cha watumishi nchini kwa kuwa malalamiko yamekuwa mengi.
Akijibu swali hilo, Waziri Kikwete ametaja maboresho yaliyofanyiwa ni malipo ya mkupuo kutoka asilimia 33 hadi asilimia 40 kwa waliokuwa wanalipwa asilimia 50, na kutoka asilimia 33 hadi 35 kwa waliokuwa wanapata asimilia 25 kabla ya kuunganisha Mifuko mwaka 2018.
Pia, amesema Januari 2025, Serikali imeongeza kima cha chini cha pensheni kutoka sh. 100,000 hadi sh. 150,000 kwa mwezi.
Vile vile, amesema serikali imehuisha pensheni ya kila mwezi kwa kiwango cha asilimia mbili kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizopo.
“Pamoja na hilo, naomba kulijulisha Bunge kuwa, Serikali itaendelea kufanya tathimini ya kupima uhimilivu wa Mifuko kila baada ya miaka mitatu kama inavyoelekezwa kisheria ili kuangalia uwezo wa kuboresha mafao bila kuathiri uendelevu wake,”amesema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED