La Vijana 600 kunolewa kwa ‘Jenga Tanzania Bora’, idadi ifike maelfu!

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 11:47 AM Feb 07 2025
Kijana
Picha: Mtandao
Kijana

SERIKALI imepanga kuwatumia vijana waliopata mafunzo na kurasimisha ujuzi katika kada mbalimbali kusaidia katika ukarabati wa miradi mbalimbali nchini.

Patrobas Katambi, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, alisema hayo wakati akijibu maswali bungeni, jijini Dodoma.

Alibainisha kuwa  vijana zaidi ya 600 wamepatiwa ujuzi katika mradi ya ‘Jenga Kesho iliyo Bora (BBT)’.

Alisema kada ambazo zimepatiwa mafunzo, ni pamoja na fundi seremala, ufundi uashi, ujenzi na zaidi ya vijana 500, wamepatiwa vyeti baada ya kuhitimu.

Akasema huo ni mpango wa kuboresha mazingira ya kisera kuwawezesha vijana kushiriki katika shughuli za maendeleo na kuweza kujitegemea, kupitia Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana na Sera ya Taifa ya Ajira.

Niipongeze serikali kwa mpango huo, pamoja na mheshimwa Katambi kwa kujibu swali hilo kwa ufasaha na kueleweka kirahisi mno.

Ushauri wangu ni kwamba, serikali iangalie zaidi kuwasaka vijana wenye vipaji zaidi kwa ajili ya mafunzo hayo.

Nikisema wenye vipaji, nina maana halisi ya kiti hicho. Wapo vijana wanaweza kupata mafunzo awali wakiwa hawajui lolote kuhusu wanachokwenda kujifunza, lakini baada ya mafunzo wakawa mafundi wazuri tu.

Lakini wapo ambao wana vipaji wa jambo husika kabla ya kwenda kujifunza.

Iwapo mradi ya Jenga Kesho iliyo Bora (BBT), itaweza kuwapata vijana wa aina zote mbili, wa kawaida na wale wenye vipaji husika, basi kuna manufaa makubwa ambayo taifa letu litapata baadaye.

Katika dunia hii, Mungu amewaumba binadamu kila mmoja na kipaji chake, lakini kwa sasa inaonekana wenzetu nje ya nchi hasa huko tunakoendelea, wamekuwa wakitumia zaidi vipaji vya wananchi wao kuziendelea nchi zao.

Maendeleo ya sayansi ya teknolojia tunayoyaona sasa yanatokana na kuwa na watu ambao wamewachukua bado wadogo baada ya kuona vipaji vyao, hivyo kuwaendeleza kimafunzo.

Yeyote mwenye kipaji fulani, akiendelezwa, anakuwa si tu anafahamu alichojifunza, lakini pia anakuwa mbunifu, na hata akifanya akipata kazi, anaifanya kwa moyo, kujitolea na kujituma kwa sababu anafanya kitu ambacho anakipenda.

Wanafanya kazi hizo mara nyingi hawajali sana maslahi yao binafsi, bali kusaidia watu, pamoja na manufaa ya nchi.

Anayefanya kazi ambayo msingi wake ni kipaji, mara nyingi hachoki, kwani hatumii nguvu nyingi kufanya na kufikiri, hivyo taifa na wananchi wake wananufaika na uwezo wake.

Tunaona wenzetu ambao wanatengeneza ndege, magari, vyombo vikubwa vya usafiri, vifaa vya ulinzi na usalama, msingi wote huo ni kupatikana kwa watu sahihi wenye vipaji, ambao wanachukuliwa na kuanza kupatiwa mafunzo sahihi na kwa wakati sahihi.

Kwa maana hiyo, naishauri BBT, ijielekeze humo, na niwaibie siri tu mara nyingi vipaji huwa kwa watu ambao wametoka kwenye mazingira au familia za kimasikini.

Mfano mdogo tu, angalia hata kwenye soka, au muziki, huwezi kukuta, mtoto anayetoka familia ya kitajiri anakuwa mwanamuziki, au mchezaji soka. Na kama wapo ni wachache mno, na hawawezi kuwa wanamuziki au wachezaji mahiri.

Hii ndiyo hata kwenye nyanja zingine. BBT, iende ndani zaidi isake pia vijana wa kimasikini wenye vipaji mbalimbali, kama ushonaji, ufundi, na vitu vingine vinavyofanana na hivyo ili hata kama ikipata wahitimu.

Basi wawe na wahitimu siyo wenye uwezo wa kushona, ufundi seremala, au fundi makenika tu, bali kupata wabunifu ambao wanaweza kufanya kitu ambacho nchi ikatikisika na kunufaika naye. Hawa watoto au vijana wapo, ila tu hawafikiwi kirahisi. Kama jitihada zitafanyika kuwasaka watapatikana na baada ya miaka kadhaa, nchi itajivunia nao kupitia mradi huo wa BBT.