BUNGE limetoa maazimio matano kuhusu uzalishaji wa sukari na mafuta ya kula nchini baada ya kubaini hautoshelezi na kusababisha kuagizwa kwa shehena za bidhaa hizo nje ya nchi.
Akiwasilisha jana bungeni taarifa ya mwaka ya utekelezaji wa majukumu ya Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Deodatus Mwanyika, alisema kutokana na kutopatikana kwa sukari ya kutosha kunaweza kusababisha upungufu.
Pia alisema kutowafikia watumiaji kwa wakati, kutasababisha bei kuwa juu, hivyo Bunge linaazimia serikali iendelee kuhamasisha uwekezaji wa viwanda vya sukari ili kuongeza uzalishaji.
Mwenyekiti huyo alisema Bunge linaazimia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) uwezeshwe kununua, kutunza na kusambaza sukari pindi uhaba unapotokea.
Pia alisema kamati inaishauri serikali kuendelea na mikakati ya kuhakikisha sukari ya kutosha inazalishwa nchini ili kupunguza kutegemea kutoka nje ya nchi na kuzalisha bidhaa zaidi ya moja, yaani sukari, umeme na ‘methanol’.
“Serikali ihakikishe miundombinu ya barabara za mashambani na ya umwagiliaji katika mashamba ya miwa ya wakulima wadogo inatengenezwa ili kurahisisha usafirishaji. Pia kamati inashauri uwekezaji ufanyike ili uzalishaji wa sukari ya viwandani ufanyike hapa nchini,” alisema.Kuhusu hali ya mafuta ya kula nchini, Mwanyika alisema bado kuna upungufu unaosababishwa na wakulima wengi kusitisha kilimo cha alizeti kutokana na kukosa soko la uhakika.
Alisema upungufu huo unasababisha wafanyabiashara kuingiza shehena kutoka nje ambayo huuzwa kwa bei ya juu.
“Bunge linaazimia serikali iendelee kuhamasisha, kuendeleza na kujenga viwanda vya kutosha vya kuzalisha mafuta ya kula nchini ili kupunguza utegemezi wa uingizaji wa mafuta ya kula na kujihakikishia usalama wa chakula nchini,” alisema.
Pia alisema Bunge linaazimia serikali iendelee kupitia upya vivutio ilivyotoa kwa wazalishaji wa ndani wa mafuta ili kuondoa athari zilizojitokeza kwa wakulima wa alizeti.
Kadhalika, alisema alizeti kama ilivyo kwa mazao mengine, iwekewe bei ambazo zitawavutia wakulima kuhamasika kulima kwa wingi.
Kuhusu tasnia ya chai, Bunge limeazimia serikali ikamilishe haraka majadiliano na wawekezaji wa viwanda ambao wameshindwa kuendesha mashamba na viwanda kwa lengo la kuwapa wawekezaji wengine wenye uwezo.
Aidha, alisema serikali ipitie upya mfumo wa uendeshaji wa mashamba na viwanda hivyo kwa nia ya kuwahusisha wakulima wadogo na wa kati kwenye uendeshaji na umiliki.
Katika hatua nyingine, Mwanyika alisema kamati haijaridhishwa na mchakato wa uanzishwaji wa mamlaka za usimamizi wa shughuli za maendeleo za sekta ya mifugo pamoja na sekta ya uvuvi.
Aliitaka serikali kuona umuhimu wa kukamilisha sehemu iliyobaki ili mamlaka hizi zianzishwe kutekeleza majukumu yake na kupata tija iliyokusudiwa kwenye sekta husika.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED