Waziri: Tunajipanga kukabili hatua za Trump

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 11:03 AM Feb 07 2025
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
Picha: Mtandao
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa msimamo wa serikali baada ya mabadiliko makubwa ambayo Serikali ya Marekani imefanya katika sera yake ya mambo ya nje, Tanzania ikijielekeza kujiimarisha na kuwa na uwezo wa ndani.

Amesema ni muhimu pamoja na upana wa uhusiano ambao wameweka, kuhakikisha wanajiimarisha na kuwa na uwezo wa ndani na hawaendelei kuwa tegemezi.

Majaliwa alisema hayo jana bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Mbozi, George Mwenisongole akiyetaka kujua serikali inajipanga vipi na mabadiliko ya Sera za Nje ya Nchi ya Marekani ambao tangu Rais Donald Trump aingie madarakani, wamefanya mabadiliko makubwa kuhusu sera hiyo.

Mbunge huyo aliuliza mabadiliko hayo yanakwenda kuathiri vipi utekelezaji sera Tanzania kwenye elimu, afya na kiuchumi ikiwamo miradi inayofadhiliwa na USAID, PP4R na programu ya kupunguza makali ya VVU/UKIMWI.

Akijibu swali hilo, Majaliwa alisema ni kweli serikali inaheshimu sera ya mambo ya nje na kutekeleza mikataba kama ambavyo walivyokubaliana na nchi husika.

Waziri Mkuu alisema wameanza kuona nchi zenye uwezo mkubwa, ikiwamo Marekani, zikibadilisha sera zao na kuathiri baadhi ya nchi na hata Tanzania inaweza kuzipata.

“Kwetu sisi ni muhimu kuzingatia sera za nje kama tulivyokubaliana. Ninampongeza Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ameendelea kufanya nchi hii kuwa na uhusiano na nchi nyingi duniani, Marekani ikiwa mojawapo.

“Muhimu kwetu sisi pamoja na upana huu wa uhusiano ambao tumeuweka, ni kuhakikisha kwamba tunajiimarisha na kuwa na uwezo wa ndani kwa kuhakikisha kwamba hatuendelei kuwa tegemezi.

“Lazima tujiimarishe kwenye mipango yetu, bajeti zetu ziweze kumudu na kutekeleza maeneo yote muhimu ikiwamo hiyo sekta ya afya, elimu maji na maeneo mengine kadri tulivyokubaliana na nchi husika," alisema.

Majaliwa alisema kama nchi, wana uwezo na zipo maliasili na rasilimali, kazi ambayo wanayo ni Watanzania kuhakikisha wanazitumia kujenga uchumi wa ndani na kuwezesha bajeti kutekeleza hayo.

“Marekani wameshatangaza, inawezekana na nchi nyingine ikatangaza kukawa na mabadiliko. Na sisi tunaendelea kujiimarisha kuhakikisha tunakuza uchumi wetu kupitia vyanzo vya fedha na mapato tunayaweka pamoja na kuyaingiza bungeni ili yapangiwe mpango kazi ili maeneo yaliyopungua tuweze kuyajazia," alisema.

Waziri Mkuu alisema huo ndio mkakati ambao sasa wako nao na ndivyo ambavyo wanajipanga kutokana na mabadiliko ambayo yanaendelea kwenye nchi zilizoendelea dhidi ya nchi ambazo zinaendelea kama Tanzania.

Hatua ya Rais Trump kutia saini agizo la kuiondoa nchi hiyo katika Shirika la Afya Duniani (WHO) siku chache zilizopita, tayari imetajwa kuanza kuleta athari kadhaa, hususan barani Afrika kama ilivyotarajiwa.

Licha ya kuwa kuna sheria zinazohitajika kufuatwa kwa taifa linalotaka kundoa ufadhili wake, utawala wa kiongozi huyo mpya tayari umechukua hatua ya kusitisha usambazaji dawa za kuzuia makali ya VVU, malaria na kifua kikuu (TB).

Athari hizo zinatokana na Marekani kuwa mchangiaji mkubwa wa kifedha wa WHO na programu mbalimbali zilizopo chini ya shirika hilo na taasisi nyingine kubwa za kiafya duniani.

Jumanne ya juma hili, makandarasi na washirika wanaofanya kazi na Shirika la Misaada la Marekani (USAID) nchini Tanzania na Kenya walianza kupokea barua hizo za kusitisha ufadhili huo mara moja, kulingana na vyanzo.

Hatua hiyo ni sehemu ya kusitishwa kwa misaada kwa Marekani na ufadhili uliowekwa tangu Trump aingie madarakani Januari 20, huku programu zikikaguliwa.

Ofisa Mkuu wa Kituo cha Kudhibti Magonjwa Barani Africa (CDC) Ngashi Ng'ongo amenukuliwa na shirika la habari la Reuters akisema nchi nyingi zimekuwa zinategemea uwekezaji wa Marekani kupitia WHO kufadhili shughuli za afya ya umma.

Kenya na Tanzania tayari USAID imetangaza kupunguza au kufuta shughuli kadhaa katika programu zake. Shirika hilo lilisema kuwa linakatiza huduma zote zilizokuwa zikitolewa na USAID kufuatia agizo la Rais Trump la kuondoa nchi hiyo WHO.