MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imeagiza kuwa Februari 19 mwaka huu, Dk. Wilbroad Slaa apelekwe mahakamani ili afuatilie kesi yake ya tuhuma kusambaza taarifa za uongo kupitia mtandao wa X.
Dk. Slaa anaendelea kusota rumande katika Gereza la Keko tangu Januari 10 mwaka huu baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kuwasilisha mahakamani hati ya kuzuia dhamana yake kwa madai ya "sababu ya usalama wake".
Agizo hilo lilitolewa jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Rahim Mushi wa mahakama hiyo wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa. Mshtakiwa hakuwapo mahakamani na hali hiyo imekuwa inatokea mara kadhaa.
Kutokana na mshtakiwa kutokuwapo mahakamani kwa mara nyingine, Wakili wa Dk. Slaa, Sanga Melikiole aliomba mahakama mteja wao awe analetwa mahakamani ili afuatilie kesi yake inavyoendelea.
"Ninaagiza Februari 19 mwaka huu mshtakiwa aletwe mahakamani ili afuatilie kesi yake," alisema Hakimu Mushi.
Awali Wakili wa Serikali, Agnes Mtunguja alidai kuwa kesi ililetwa kwa kutajwa na upelelezi haujakamilika, hivyo kuomba tarehe nyingine ya kutajwa.
Hata hivyo, Mahakama ya Kisutu imefungwa mikono kuendelea na hatua yoyote kwa sababu DPP amewasilisha kusudio la kukata rufani Mahakama ya Rufani kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu uliompa unafuu Dk. Slaa katika suala la dhamana.
Inadaiwa kuwa Dk. Slaa alitenda kosa hilo, Januari 9 mwaka huu ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia mtandao huo wa kijamii, kupitia jukwaa lililosajiliwa kwa jina la Maria Salungi Tsehai @MariaSTsehai kwa lengo la kupotosha umma.
Inadaiwa kuwa kupitia jukwaa hilo, Dk. Slaa alichapisha ujumbe uliosomeka 'wakubwa wametafutana, nikisema wakubwa namaanisha mwamba na Samia, na wala hatuna maneno ya kumung'unya... na kimsingi wamekubaliana, Suluhu Samia amekubali atatoa pesa, Suluhu Samia amekubali ataongeza nguvu ya pesa, ni dhahiri atatoa pesa... hizo ni hela za Watanzania wanazichezea Samia na watu wake.
"Samia toka muda mrefu hahangaikii tena maendeleo ya nchi, anahangaikia namna ya kurudi Ikulu na namna yake ya kurudi Ikulu ni kwa njia hizo kama kumsaidia mtu kama Mbowe".
Inadaiwa kuwa Dk. Slaa, aliyewahi kuwa Mbunge wa Karatu, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na balozi, alisambaza maneno hayo mtandaoni wakati akijua taarifa hizo ni za uongo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED