SHEKHE Ponda Issa Ponda na wenzake 11 wameomba mahakama wafanye marekebisho kwenye hati ya madai kumwondoa Yustadhi Twalib Twalib katika kesi ya kikatiba waliyofungua kupinga kuwa chini Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) kutokana na mwenzao huyo kufariki dunia.
Mbali na Sheikh Ponda, wadai wengine Shekhe Ayoub Muinge, Sheikh Prof. Hamza Njozi, Riziki Ngwali, Bakari Shingo, Juma Kilaghai, Abdallah Said, Twalib Twalib, Ibrahim Sherally, Mussa Marua, Abubakar Mngodo na Mustafa Abedib.
Ombi hilo la masheikh hao lilitolewa jana na wakili wao, Juma Nassoro mbele ya Jaji Arnold Kirekiano wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam wakati shauri hilo lilipoitwa kwa ajili ya kusikilizwa.
"Mheshimiwa Jaji, ninaomba tufanye marekebisho kwenye hati ya madai ili kumwondoa marehemu Twalib Twalib," alidai Wakili Nassoro.
Jaji Kelekiano alikubaliana na ombi hilo na kuwaelekeza kwamba marekebisho hayo wayafanye Februari 12, 2025 na upande wa wadaiwa utajibu Februari 26, 2025 na shauri litasikilizwa Machi 3, 2025.
Wadai hao mbali na Wakili Nassoro, wanawakilishwa pia na Wakili Yahaya Njama, Daimu Hafani, Abdulfattaha A-Bakry na Ubaid Hamidu.
Wamefungua kesi hiyo dhidi ya Msajili wa Vyama vya Kijamii - Wizara ya Mambo ya Ndani, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Mkabidhi wa Wasihi Mkuu, BAKWATA na Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania.
Katika hati yao, wanalalamikia kitendo cha mdaiwa wa kwanza, Msajili wa Vyama vya Kijamii na wa pili, Mkabidhi wa Wasihi Mkuu kuwalazimisha waislamu wanaotaka kusajili taasisi yoyote kuwa lazima wapate barua kutoka BAKWATA inayowatambua.
Inadaiwa kuwa katika sheria za Tanzania, hakuna sehemu yoyote inayolazimisha muislamu kuwa chini ya BAKWATA, Baraza hilo limesajiliwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na pia limesajiliwa Rita kama zilivyosajiliwa taasisi zingine. Halina usajili wa kwamba lenyewe ndiyo taasisi ya kuwakilisha waislamu wote Tanzania.
Pia wanadai katika Katiba ya BAKWATA hakuna kipengele chochote kinachoeleza nani ni mwanachama wa BAKWATA na kwamba ukitaka kuwa mwanachama wa BAKWATA, lazima uombe. Hakuna jambo hilo.
"Kwa hiyo kuwalazimisha waislamu kuwa chini ya BAKWATA ni kinyume cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Waislamu waachwe wenyewe waamue wanataka kuwa chini ya taasisi gani na wanapotaka kusajili taasisi yoyote ya kidini wasilazimishwe kutambuliwa na BAKWATA.
"Walazimishwe kwa sababu Katiba inatoa uhuru wa mtu yeyote kujiunga na jumuiya yoyote anayoitaka, huwezi kuwalazimisha wawe chini ya BAKWATA, huko ni kuvunja Katiba. Hakuna sheria inayowataka RITA au Msajili wa Vyama vya Kijamii kuelekeza waislamu waende BAKWATA wakalete barua, hakuna sheria hiyo," wanadai katika hati yao.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED