Ufadhili usambazaji nishati safi kupikia upewe msisitizo

Nipashe
Published at 10:23 AM Jan 29 2025
Ufadhili usambazaji nishati  safi kupikia upewe msisitizo.
Picha:Mpigapicha Wetu
Ufadhili usambazaji nishati safi kupikia upewe msisitizo.

Suala la upatikanaji wa nishati safi ya kupikia ni ajenda kubwa duniani kote likiwa na lengo la kuhakikisha watu wengi wanatumia aina hiyo ya nishati kwa manufaa ya kiafya, kiuchumi na kupunguza kasi ya matumizi ya mkaa na kuni kwa ajili ya kupikia pamoja na uharibifu wa mazingira.

Tangu alipoingia madarakani takriban miaka minne iliyopita, Rais Samia Suluhu Hassan ameweka kipaumbele suala hilo na amekuwa kinara katika kuhimiza matumiai ya nishati safi kwa Afrika nzima. Hatua ya Rais Samia kuipa kipaumbele ajenda hiyo ni kutokana na madhara ya kiafya na kiuchumi kwa wanadamu hasa wanawake. 

Kwa mazingira ya kawaida na maisha ya kiafrika, mwanamke ndani ya nyumba ndiye mwenye wajibu mkubwa wa kuhakikisha huduma za familia kama vile chakula, maji na nishati kupikia zinapatikana. Kwa mantiki hiyo, mwanamke hutumia muda mwingi kwa ajili ya kutafuta kuni au mkaa kwa ajili ya kupikia chakula cha familia na matokeo yake, anashindwa kufanya kazi za uzalishaji ili kujikwamua kiuchumi binafsi, familia na jamii kwa ujumla.      

Kutokana na kuwapo kwa hali hiyo, serikali imeweka kipaumbele kuhusu upatikanaji wa nishati safi ya kupikia ili kuokoa muda wa kutafuta nishati ya kupikia hasa kuni na mkaa ambayo si salama kwa afya ya mtumiaji na pia inachangia kasi ya uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi. 

Serikali, katika kutimiza ajenda hiyo ambayo inapewa kipaumbele na Rais mwenyewe, imeandaa mkakati wa miaka 10 ya nishati safi ya kupikia kuanzia mwaka 2024 hadi 2024. Kwa mujibu wa takwimu matumizi ya nishati safi ya kupikia yameongeza kwa kasi ndogo kutoka asilimia 1.5 mwaka 2010 hadi asilimia 6.9 mwaka 2021. Takwimu hizo ziko chini sana ya matumizi ya kidunia ya wastani wa asilimia 71 katika kipindi hicho.     

Hali hiyo inaonesha jitihada kubwa zinatakiwa kufanyika ndiyo maana serikali katika mkakati huo, imedhamiria kuwa asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati hiyo ifikapo wakati huo. Mkakati huo pia unaendana na lengo Namba  7 la Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG) ya Umoja wa Mataifa la kuhakikisha upatikanaji wa nishati nafuu, inayopatikana kwa urahisi, endelevu na ya kisasa kwa wote. 

Tangu kuanza kwa utekelezaji wa mkakati huo, serikali imeweka juhudi kubwa katika kuhakikisha Watanzania wengi wananufaika na matumizi ya nishati safi ya kupikia na kampuni kadhaa zinazouza nishati hiyo hasa gesi ya kupikia zimepewa nafasi ya kusambaza. Pamoja na kupewa nafasi hiyo, tatizo kubwa limekuwa uwezo wa kifedha katika kufikia azma ya kuwapatia wahitaji aina hiyo ya nishati, hivyo kuhitaji mikopo kutoka taasisi za fedha. 

Hatimaye kilio hicho kimewafikia wadau hasa taasisi za fedha kuanza kutoa mikopo kwa ajili ya usambazaji wa nishati safi. Benki ya NMB imekuwa mfano kwa kutoa Sh. milioni 100 kwa ajili ya kukopesha wasambazaji wa gesi ya kupikia kwa lengo la kufanikisha azma hiyo ya serikali.

Ni dhahiri kwamba kiasi hicho cha fedha kitachochea kasi ya usambazaji wa gesi ya kupikia kwa Watanzania wengi kupitia kampuni zilizopewa kazi hiyo kupitia mikopo yenye riba nafuu ya benki hiyo. Kwa mantiki hiyo, kutakuwa na kasi zaidi ya kupatikana kwa gesi hiyo hadi maeneo ya vijijini ambako ndiko kwenye tatizo kubwa la utumiaji wa nishati isiyo safi hasa kuni na mkaa ambayo ni hatarishi kwa afya na maisha ya watumiaji. 

Pamoja na ukweli huo, ni vyema serikali ikatoa garantii kwa kampuni zinazosambaza gesi ya kupikia pamoja na zile zinazotengeneza majiko banifu na sanifu ili zipate mkopo nafuu kupitia taasisi za fedha, hasa benki kama ilivyofanyika kwa NMB.