Mkutano wa nishati waipaisha Tanzania kimataifa

Nipashe
Published at 08:32 AM Jan 28 2025
Mkutano wa nishati waipaisha Tanzania kimataifa.
Picha: Mtandao
Mkutano wa nishati waipaisha Tanzania kimataifa.

TANZANIA imepata ugeni mkubwa wa zaidi ya marais 25, Mawaziri Wakuu na Manaibu Mawaziri Wakuu, Mawaziri wa Fedha na Nishati 60 wa Afrika, ambao wako nchini kushiriki mkutano wa Nishati wa Mission 300.

Ujio wa ugeni huo ni fahari kubwa kwa Tanzania kwa kuwa pamoja na wageni hao kushiriki mkutano huo muhimu, pia ni fursa ya kipekee ya kutangaza vivutio mbali mbali vya uwekezaji na vivutio vya utalii vilivyopo nchini.

Jiji la Dar es Salaam, ambako mkutano huo unafanyika, limekuwa na shamrashamra za kila aina kuhakikisha wageni wanaoingia wanakutana na mandhari nzuri itakayowavutia kurudi tena.  

Miongoni mwa shughuli zitakazofanyika katika mkutano huo ni pamoja na kusaini Mpango Mahususi wa Nishati wa Afrika, awamu ya kwanza utakaozishirikisha nchi 14 za Tanzania, Malawi, Chad, Nigeria, Burkina Faso, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Niger, Liberia, Msumbiji, Madagascar, Zambia, Mali, Ivory Coast na Mauritania.

Pia, utajadili namna ya kutumia fursa ya ushawishi kwa wadau wa maendeleo kutenga fedha kwa ajili ya miradi ya nishati jadidifu, ambayo ni rafiki kwa mazingira.

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, pia imesema baada ya mkutano huo, Rais Samia Suluhu Hassan anatarajia kuwa na mazungumzo na wakuu hao wa nchi kuhusu masuala ya ushirikiano na nafasi ya Tanzania katika kushirikiana na nchi hizo.

Alitaja nchi ambazo wakuu wa nchi wanashiriki katika mkutano huo kuwa ni Algeria, Visiwa vya Comoro, Malawi, Zambia, Sierra Leone, Liberia, Somalia, Lesotho, Botswana, Guinea Bissau, Kenya, Burundi, Mauritania, Congo Brazzaville, Madagascar, DRC Congo, Libya, Khartoum Sudan, Ethiopia, Nigeria, Ghana, Djibout, Togo na Gabon.

Viongozi wengine wanaohudhuria ni Makamu wa Rais wa Gambia, Makamu wa Rais wa Benin, Waziri Mkuu wa Ivory Coast, Waziri Mkuu wa Uganda, Waziri Mkuu wa Visiwa vya Sao Thome, Waziri Mkuu wa Equatorial Guinea, Naibu Waziri Mkuu wa Ufalme wa Eswatini, Naibu Waziri Mkuu wa Namibia.

Kuna mawaziri mbalimbali, manaibu waziri wakuu na  Afrika Kusini imewakilishwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati wa nchi, Waziri wa Nishati, Viwanda na Madini wa Tunisia, Waziri wa Mambo ya Nje wa Falme za Kiarabu, Waziri wa Nishati kutoka Rwanda, Waziri wa Nishati Morocco, Waziri wa Nishari Zimbabwe na Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Pia, yupo Rais kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika Dk. Akinwumi Adesina na Rais wa Benki ya Dunia, Ajay Banga.

Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) anayeshughulikia masuala ya nishati na mabadiliko ya hali ya hewa, Dk. Kevin Kariuki, amesema mkutano huo ni muhimu kwa kuwa unakutanisha wakuu wa nchi na viongozi wengine ambao baada ya kujadiliana, watasaini Azimio la Dar es Salaam.

Azimio hilo litaweka makubaliano yaliyofikiwa kutekelezwa kuhusu mkutano huo muhimu na viongozi hao watashuhudia wakikubaliana na kuingia mkataba wa kuwezesha lengo la kusambaza umeme kwa watu milioni 300 kabla ya 2030 kufikiwa.

Ujio wa viongozi hao na ujumbe wao unatoa fursa kwa wafanyabiashara nchini kutangaza bidhaa zao na vile vile, hoteli nyingi zimepata wageni ambao watasaidia kuingiza fedha za kigeni.