WIKI hii, Idara ya Uhamiaji, ilithibitisha kuwapa uraia wachezaji watatu wa Singida Black Stars, Emmanuel Kwame Keyekeh, Josephat Arthur Bada na Mohamed Damaro.
Taarifa kutoka kwa Msemaji, Mkuu wa Idara ya Uhamiaji, Paul Mselle, ilithibitisha wachezaji hao kupatiwa uraia wa Tanzania.
Taarifa ilisema wachezaji waliomba na walipewa kwa mujibu wa vifungu vya 9, 23 vya Sheria ya Uhamiaji, sura ya 357. Na kwamba wamepewa uraia wa Tanzania kwa Tajnisi.
Hata hivyo, utoaji huo wa uraia ulizua mjadala mkubwa, si kwa wapenzi, wadau na mashabiki wa soka pekee, bali hata kwa raia wa kawaida na watu wa kada zingine, wakiwamo wanasheria.
Wengi walidhani kuwa wachezaji hao, Keyekeh raia wa Ghana, Bada wa Ivoct Coast na Damaro, akitokea Guinea, bado hawakuwa na vigezo vinavyowawezesha kuwa raia wa Tanzania kwa mujibu wa sheria.
Hata hivyo, hatupo hapa kubishana na mamlaka kwa sababu yenyewe ndiyo yenye uamuzi wa mwisho wa kutoa uraia kutokana na vigezo vyao wanavyoona vinakidhi sheria. Lakini kama imetoa kwa sababu za kimpira ili walisaidie taifa kama ambavyo inatajwa, basi kutakuwa na maswali ya kujiuliza.
Kwanza, Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Hemed Morocco, amewahitaji wachezaji hawa ili baadaye awajumuishe kwenye kikosi hicho baada ya kujiridhisha kuwa na vipaji maalum?
Kama si hivyo, kocha Morocco alisiporidhika nao na kutowaita kwenye kikosi cha timu ya taifa? Tuna uhakika mpaka kufikia CHAN na AFCON, wachezaji hawa watakuwa kwenye kiwango kichachotakiwa cha kuichezea Stars?
Tunaamini kama wamepewa kwa sababu ya 'uspesho' wao kwenye soka na kuwa watalisaidia taifa, lakini sheria ya FIFA zinapinga hilo, hivyo hawatocheza CHAN wala AFCON, ndiyo maana tunaona kuna shida sehemu.
Tunasema si rahisi kucheza kwa sababu kwa mujibu wa sheria za FIFA ni kwanba. Mchezaji aliyebadili uraia ili kuichezea nchi husika, anapaswa kuishi kwenye nchi yake mpya kwa miaka isyopungua mitano ili apate sifa ya kuichezea timu ya taifa, sifa ambayo wachezaji hao wanaikosa.
Lakini pia mchezaji anapaswa kuwa amesafiri kwenye nchi yake hiyo mpya akiwa na umri wa miaka 10 na 18, huku FIFA wakihitaji ushahidi wa tiketi, visa, vibali vya ukazi vyenye tarehe sahihi.
Tatu, FIFA watachunguza kama sababu ya kubadili uraia mchezaji haikuwa ya kimpira, yaani wakigundua alibadili ili achezee timu ya taifa, hawatoi ruhusa hiyo. Kwa vigezo hivyo vyote tuna wasiwasi kama wanaweza kuwa navyo, hivyo watakuwa wamepewa tu kama zawadi, huku wakipata bahati ya mtende ya kutokidhi vigezo vingi, zaidi ya uamuzi wa mwisho wa mamlaka.
Hapa ndipo linapokuja swali lingine. Je suala hili kweli limefanywa kwa ajili ya manufaa ya timu ya taifa, au klabu ya Singida Black Stars? Kwa nini wachezaji walioomba uraia wawe kutoka klabu moja tu?
Tunaona kama hili litakuwa limefungua mlango kwa klabu nyingi za Tanzania kuwashawishi wachezaji wao kuomba uraia kwa kutumia vigezo kama ambavyo vimetolewa kwa hao waliopewa.
Tayari wachezaji tisa wa Simba wameomba wapewe uraia kwa sababu hizo hizo ambazo wa Singida Black Stars wamesababisha wapewe. Klabu ya Simba imethibitisha hilo, ikiwa nyuma ya wachezaji wake kutaka wapatiwe uraia kama walivyopewa wenzao.
Huu ni mtego ambao umeingiwa. Vyovyote itakavyokuwa, kama ikikubali, basi nchi hii itakuwa na raia wengi ambao ni wachezaji, kazi yao kubwa ikiwa ni mpira, kazi ya muda mfupi, wakistaafu wanajazana hapa hapa.
Pili klabu zitakuwa zinatumia njia hii kukwepa kulipa vibali vya kazi na kuishi nchini, hivyo itakuwa ni hasara tu kwa taifa ambalo lilikuwa liingize mapato yake kupitia sekta hiyo ya michezo.
Tatu kwa utaratibu huo wa kutoa uraia kwa wachezaji kupitia klabu, zinaweza kufanya hivyo kila msimu wa usajili kwa wale waliopewa wanaposhuka viwango, hivyo tunaona mamlaka husika imefungua mlango ambao unaweza kuwa mgumu kuufunga.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED