CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimemaliza uchaguzi wa viongozi wake wakuu katika mkutano mkuu uliofanyika kuanzia Januari 20 na kutamatika mapema jana.
Katika uchaguzi huo, mwanasiasa na mwanasheria machachari, Tundu Lissu, ameibuka mshindi katika nafasi ya mwenyekiti baada ya kumbwaga aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo kwa zaidi ya miongo mwili, Freeman Mbowe. Lissu alipata kura 513 sasa na asilimia 51.5 wakati Mbowe alipata kura 483 ambazo ni asilimia 48.3.
Naye aliyekuwa Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche, amekuwa makamu mwenyekiti wa chama hicho kikuu cha upinzani akichukua nafasi ya Lissu aliyekuwa akiishikilia nafasi hiyo kabla ya uchaguzi.
Kwa kuangalia takwimu za matokeo hayo ya mwenyekiti, inaonesha dhahiri kwamba ushindani ulikuwa mkubwa kama ilivyoonekana wakati wa mnyukano wa hoja na kuwapo kwa makundi ya wafuasi wa pande mbili kabla ya kwenda kwenye sanduku la kura. Kwa maneno mengine, haikuwa rahisi kutabiri mshindi baina ya vigogo hao wa siasa ndani ya CHADEMA.
Baada ya matokeo kutangazwa na mshindi kujulikana, Mbowe aliandika katika mtandao wake wa X kuwa anakubali kushindwa na kumpongeza mpinzani wake kwa ushindi alioupata. Huo ndio uungwana wa kisiasa kwa mtu kukubali kushindwa badala ya kuanza kuibua nongwa ambazo zinaweza kukigawa chama na hata kuonesha kuwa mtu si mwanademokrasia kama anavyoinadi majukwaani.
Hatua hiyo ya ukomavu wa demokrasia ndani ya CHADEMA imepongezwa na watu wengi wakiwamo wanasheria na wanaharakati wa haki za binadamu kwamba umekuwa wa huru na wa wazi.
Mmoja wa wanaharakati waliopongeza hatua hiyo ni Mkurugenzi Mtendaji mstaafu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Hellen Kijo-Bisima, aliyesema hatua iliyofikia CHADEMA katika uchaguzi huo ni ukomavu wa siasa kwa kuwa umekuwa wa amani. Zaidi ya hayo, amesema mshindi amepatikana na aliyeshindwa amekubali kushindwa na hiyo ndiyo maana halisi ya demokrasia.
Mwenyekiti huyo mteule kwa upande wake, baada ya kutangazwa mshindi alisema chama kimeweka kiwango cha dhahabu cha demokrasia ya ndani na kuvitaka vyama vingine vya siasa nchini kuiga mfano wao. Pia alibainisha kuwa uchaguzi ulikuwa wa wazi, huru na haki bila mizengwe japo alikiri kuwa kulikuwa na misuguano na kasoro za hapa na pale.
Katika kuonyesha kwamba wataendelea kuwa wamoja, Lissu alisema Mbowe ndiye aliyefanikisha uchaguzi huo kuwa katika hali hiyo na anastahili pongezi huku akiweka bayana kwamba historia ya chama itakapoandikwa, watu watatambua huu mchango wake mkubwa aliotoa. Pia alisema Mbowe hajastaafu bali ataendelea kuwa mjumbe wa kudumu wa kamati kuu ya chama kama katiba ya CHADEMA inavyoainisha.
Wahenga siku zote wanasema hakuna adui wa kudumu wala rafiki wa kudumu katika siasa, hivyo baada ya minyukano na kuibuka kwa makundi ya wapambe waliokuwa wanatukana na kukejeli upande mwingine, CHADEMA hawana budi kuondoa tofauti zao na kurejea kukijenga na kukiimarisha chama chao.
Jukumu kubwa linalopaswa kufanywa na makundi hayo, yaliyokuwa yakijulikana kama ‘Team Mbowe’ na ‘Team Lissu’ ni kuungana na kuwa wamoja hatimaye kuendelea kukifanya kuendelea kuwa chama kikuu cha upinzani. Pia wana CHADEMA wanapaswa kuudhirihishia umma kwamba maneno yaliyokuwa yakienezwa kwamba chama kitasambaratika, zilikuwa ndoto za mchana na kwamba kitaendelea kuwa imara zaidi kuliko awali.
Pia viongozi, wanachama na wafuasi wa CHADEMA wanapaswa kutambua kwamba uchaguzi ndani ya chama umetamatika hivyo kazi iliyobaki ni kujijenga chama na kujiandaa na uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika Oktoba, mwaka huu na hatimaye kushinda.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED