Biteko aongoza harambee ujenzi Jimbo Katoliki Rulenge-Ngara

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 01:23 PM Feb 23 2025
Naibu  Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko
Picha: Mpiagapicha Wetu
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, amempongeza Askofu wa Jimbo Katoliki Rulenge-Ngara, Mhashamu Severine Niwemugizi, kwa maono ya kujenga Kanisa Kuu la Jimbo Katoliki hilo, mkoani Kagera.

Dk. Biteko ametoa pongezi hizo jijini Dar es Salaam, wakati aliposhiriki katika harambee ya ujenzi wa kanisa hilo.

“Nakupongeza Baba Askofu kwa kuwa na maono makubwa ya kujenga hekalu la bwana la viwango vya juu na kuwaza makubwa,” amesema Dk. Biteko.

“Binafsi namuona Baba Askofu kama mbeba maono wa Jimbo na sisi tumshike mkono, ili nia yake iweze kufanikiwa. Kiu hiyo itafanikiwa kwa kuwa nia ipo na kanisa litajengwa na sisi wenyewe,” aliongeza.

Dk. Biteko amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan, wa kumpa fursa ya kumwakilisha kushiriki katika tukio hilo la harambee ya ujenzi wa kanisa.

Askofu wa Jimbo Katoliki Rulenge-Ngara, Mhashamu Niwemugizi, amesema kuwa jimbo hilo liliundwa mwaka 1960 na kwa sasa linajumuisha Wilaya za Biharamulo, Chato na Ngara.

Askofu wa Jimbo Katoliki Rulenge - Ngara, Mhashamu Severine Niwemugizi akihubiri katika ibada maalum ya kuombea harambee ya ujenzi wa Kanisa Kuu la Jimbo Katoliki la Rulenge - Ngara mkoani Kagera, misa hiyo iliongozwa na Mhadhama Protase Rugambwa
Ameongeza kuwa Kanisa lililopo lilianza kama kigango na limekuwa likipanuliwa mara kwa mara, kulingana na mahitaji, hivyo wamefikia uamuzi wa kujenga kanisa jipya, ili kukidhi mahitaji ya sasa.

Awali akizungumza wakati wa misa takatifu, Askofu Niwemugizi, amemshukuru Rais Samia, kwa kukubali kuwasaidia kufanya harambee kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa Kuu la Jimbo Katoliki la Rulenge-Ngara, mkoani Kagera na kuwa hatua hiyo, inadhihirisha upendo upendo wa dhati wa Rais kwa wananchi wa Ngara na Watanzania kwa ujumla.

“Katika kujenga nyumba ya bwana tulipopiga hodi kwa Rais Samia kumuomba atusaidie kujenga nyumba ya heshima ya bwana alikubali na tunafurahi jioni hii amemtuma Dk. Biteko awe nasi.

“Tumtukuze Mungu katika ushirikiano huu anaouweka na kwamba viongozi wa serikali wako tayari kusaidia watu katika kutimiza nia zao,” amesema Askofu Niwemugizi.

Harambee ya ujenzi wa Kanisa Kuu la Jimbo Katoliki la Rulenge - Ngara mkoani Kagera,
Mhandisi wa mradi wa ujenzi wa Kanisa hilo, Daudi Masaka, amesema kuwa ujenzi wa kanisa hilo hadi kukamilika kwake utagharimu jumla ya Sh. bilioni 7.7.

Aidha, ametaja baadhi ya sehemu ya kanisa hilo, kuwa sakafu ya pili ya jengo litakuwa na uwezo wa kubeba watu 2100, makanisa madogo mawili na sehemu ya makaburi manne.

Aidha, harambee hiyo imehudhuriwa pia na viongozi mbalimbali akiwamo Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba.