Endelezeni elimu ya dini - Majaliwa

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 02:42 PM Feb 23 2025
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliingia uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliingia uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa ametoa wito kwa viongozi wa madhehebu ya dini kuendelea kufundisha na kuimarisha elimu ya dini ili kutoa fursa kwa watoto na vijana kupata elimu hiyo na kuwaandaa kuwa watu wenye maadili mema.

Majaliwa ametoa wito huo leo Jumapili Februari 23, 2025 alipomwakilisha Rais  Samia Suluhu Hassan kwenye kilele cha Tuzo za 33 za Kimataifa za Kuhifadhi Qurani tukufu, yanayofanyika katika uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Kiongozi  huyo amesema jukumu la kuhakikisha maadili bora ni la kweo sote, huku madhehebu ya dini yakiwa na mchango mkubwa.

"Nihimize madhehebu yote ya dini kuendelea kuhubiri amani, mshikamano na utulivu hasa katika kipindi cha kuelekea katika uchaguzi Mkuu. Amani na utulivu ni moja ya tunu katika nchi yetu," amesisitiza Majaliwa.

Ameongeza tuzo hizo pia zinatoa nafasi ya kujenga maadili bora ikiwemo uaminifu, umakini, na kujitolea. “Washiriki wanajifunza umoja, upendo na mshikamano na wengine kwa ufanisi.

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema kuwa mashindano hayo yanahamasisha jamii ya Kiislamu duniani kote kuwa na utamaduni wa kujisomea na kuhifadhi Qur'aan tukufu.

“Hii inachangia kuendeleza utamaduni wa kuheshimu dini, kudumisha maadili mema, amani na kuimarisha imani katika jamii," amesema Majaliwa.

“Mashindano haya yanawawezesha vijana na watoto kuonesha uwezo wao katika usomaji na uhifadhi wa Qur'aan Tukufu. Hii ni fursa muhimu kwao kukuza kipaji, kujivunia mafanikio yao, na pia kujenga nidhamu na uwajibikaji," amesema Majaliwa.

Pia amesema serikali inaamini mashindano hayo yatasaidia kuleta maendeleo ya kiroho kwa vijana na kuhamasisha jamii kwa ujumla, akiahidi kuwa mamlaka itaendelea kushirikiana na jumuiya na taasisi mbalimbali katika kukuza na kuhamasisha shughuli za kidini nchini.