CCM imeonesha ukomavu kwa miaka 48 ya uhai wake

Nipashe
Published at 08:27 AM Feb 06 2025
CCM imeonesha ukomavu  kwa miaka 48 ya uhai wake.
Picha: Mtandao
CCM imeonesha ukomavu kwa miaka 48 ya uhai wake.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) jana kiliadhimisha miaka 48 tangu kuanzishwa mwaka 1977. Chama hicho kilianzishwa baada ya kuunganishwa TANU, chama kilichopigania na kupatikana kwa Uhuru wa Tanganyika (Tanzania Bara) na Afro Shiraz Party (ASP) kilichopigania na kufanikisha Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar mwaka 1964.

Tangu kuanzishwa hadi sasa, CCM imekuwa na utaratibu wa kuchagua viongozi kila baada ya miaka mitano ndani ya chama, hivyo kuonesha kwa dhati kuwa kinadhihirisha demokrasia ya kweli na kuwa chama kiongozi katika kutekeleza jambo hilo na utawala wa sheria. 

Kila unapofika wakati wa uchaguzi ndani ya chama, hufanyika mchakato kwa wanachama kuomba nafasi na majina ya waombaji kujadiliwa katika vikao mbalimbali na hatimaye wenye sifa kupitishwa kwa ajili ya kugombea katika uchaguzi mkuu kwenye ngazi husika.

Licha ya kufanya uchaguzi na kuwezesha viongozi kubadilishana na kupozana madaraka kwa njia ya ushindani wa wazi, CCM pia imekuwa mfano bora si kwa Tanzania tu bali kwa Afrika kuwa chama chenye nia ya dhati ya kudumisha demokrasi na utawala bora. Viongozi wa juu, kwa maana ya Rais wa Tanzania na Zanzibar, wakimaliza vipindi viwili vya miaka mitano kila kimoja, huachia madaraka na kupisha wengine kuwania nafasi za urais kwa njia ya ushindani.

Katika muktadha huo, tangu kuanza kwa uchaguzi mkuu unaohusisha vyama vingi mwaka 1995, kumekuwa na idadi kubwa ya wanachama wanaojitokeza kwa wingi kwa ajili ya kuwania nafasi hiyo. 

Mwaka 2005 kwa mfano, walijitokeza wanachama 11 kuwania nafasi ili kumrithi aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa. Pia mwaka 2015, walijitokeza wanachama 28 kumrithi Jakaya Kikwete, hali ambayo inaonyesha kukomaa kwa demokrasia ndani ya chama hicho tawala. Hali hiyo ni tofauti na baadhi ya vyama ambavyo vimekuwa ama vikipendekeza mtu mmoja kuwa mgombea au kiongozi mkuu wa chama husika kujitangaza kuwa ndiye mgombea.

Mbali na demokrasia, CCM imekuwa ikikemea rushwa na kufuatilia kwa kina utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi katika kipindi husika kupitia miradi ya maendeleo ya uondoshaji wa kero za wananchi. Mwaka 2013, kwa mfano, sekretarieti ya CCM iliyokuwa chini ya aliyekuwa Katibu Mkuu, Abduklrahman Kinana, ilizunguka nchi nzima na kukutana na kero mbalimbali zinazowakabili wananchi.

Kutokana na kuwapo kwa kero hizo, viongozi hao waliwaita baadhi ya mawaziri ambao kero zilihusu wizara zao na kuhojiwa kwa nini mambo hayo yanaendelea na hakuna hatua zinazochukuliwa. Hali hiyo pia ilisababisha mawaziri waliokuwa wakihusishwa na kero hizo, kuitwa ‘mawaziri mizigo’, hivyo kupendekeza kwa Rais kuwachukulia hatua. 

Pamoja na hayo, CCM imeendelea kusisitiza viongozi wanaopewa dhamana kutatua kero za wananchi badala ya kudhani kuwa wako kwenye nafasi hizo kwa manufaa binafsi. Hiyo imekuwa ikisisitizwa kuanzia ngazi ya taifa hadi mtaa na kijiji kila kiongozi awajibike kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo.

Kwa ujumla, CCM imedhihirisha kuwa imekomaa katika kudumisha demokrasia, utawala bora, haki na usawa kwa wananchi  bila kujali itikadi na imani zao. Kwa sasa, kutokana na kusimamia maendeleo ya wananchi katika sekta mbalimbali, CCM imeonesha kuwa bado kimbilio la wengi katika maendeleo ya nchi. Hali hiyo imejidhihirisha katika uchaguzi mbalimbali kwa kushindwa kwa kishindo.

Wahenga wanasema barabara ndefu haikosi kona. Ni ukweli kwamba chama hicho kimeonesha kuwa kikongwe lakini kuna kasoro kadhaa ambazo zimekuwa zikikwamisha uhuru na demokrasia. Hata hivyo, kasoro hizo haziifanyi kionekana chama dhaifu kulinganisha na vingine vilivyoasisiwa rasmi kuanzia mwaka 1992 baada ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi.