HIVI karibuni mwimbaji wa nyimbo za Injili Rehema Simfukwe na mumewe Isaya Lyimo, wameikabili dhana potofu kuwa watoto wenye usonji wana tofauti na wengine wenye fahamu na utimilifu wa kimaumbile.
Wamelithibitisha hilo baada ya kumuonesha mtoto wao wa kwanza, Dorcas Lyimo (6), hadharani bila kuwa na hofu wala kudhani watu watasemaje kwa kuwa ana changamoto za kimaumbile.
Hali hii huenda haijawahi kuwa rahisi kwa wazazi wake kuipokea, wamepitia mengi katika malezi ya binti yao huyo ambaye ndiye uzao wao wa kwanza. Pamoja na changamoto zote hawakukata tamaa katika kuhakisha anapatiwa mahitaji muhimu na malezi bora.
Wazazi wake wameielezea jamii historia yake ambayo hatukuifahamu hapo awali, pia wameamua kuanzisha kituo ambacho kitawasaidia wototo wengine wenye tatizo kama la Dorcas, ambacho kimepewa jina la Dorcas Home Care.
Kituo hicho kimezinduliwa rasmi katika maadhimisho ya siku yake ya kuzaliwa ili watoto walio na usonji wanufaike.
Ukweli ni kwamba walio wengi wenye tatizo kama hili wamekuwa wakifichwa ndani na kuwakosesha haki zao za muhimu kama watoto wasio na changamoto.
Pia, wamemuandalia kitabu ambacho kitaelezea historia yake tangu alipozaliwa, hadi sasa ili kueleza jamii yale aliyoyapitia na njia walizochuka wazazi wake na kumfanya kuwa ni mtoto mwenye furaha kama ilivyo kwa wengine.
Naona lipo la kujifunza wazazi wenzangu kutokana na tatizo alilolipata mtoto huyu, kwani kumekuwa na mtazamo hasi kwa jamii pale anapozaliwa mtoto mwenye tatizo la usonji.
Kutokana na imani potofu ndizo zinazowafanya watoto hawa kujiona wana utofauti na wengine, pia kuwa wanyonge kutokana na unyanyapaa wanaupata kutoka kwa baadhi ya watu wa karibu na hata kwa wanafamilia na jamii nzima.
Wazazi, walezi wenye watoto kama Dorcas mnapaswa kuwapenda, kuwajali na kuwapa kila wanachostahili ili kukua na kufanikiwa kwenye maisha yao ili kuwapa furaha na si kujihisi kuwa wana utofauti wakijilinganisha na wengine wasiokuwa na changamoto hiyo.
Ili mzazi uweze kumtambua mtoto wako kama ana usonji, ni vema uwe karibu naye kwa kuzingatia malezi kwani itakurahisishia kutambua kama mtoto ana changamoto hiyo kwakuwa zipo dalili ambazo kama mzazi au mlezi ukiziona utatambua na kumsaidia.
Dalili ya kwanza mtoto kupata shida hiyo ni kushindwa kuwasiliana na kushirikiana na watu , hali inayomuanza tangu udogoni. Anashindwa kuwatizama machoni mama yake, wanafamilia na wengineo wanaomzunguka.
Anafanya mambo yasiyo ya kawaida tena kujirudia, dalili hizi zinaanza katika umri mdogo, mara nyingi wakati mtoto akiwa bado mchanga. Wengine wanaweza kusema hatulii au ni mtukutu hasa anapoanza kutembea na kushika na kuchezea vitu.
Vile vile mtoto anakuwa mzito kuanza kuzungumza au anashindwa kujifunza kuzungumza, anazidi kuogopa kukutanisha macho yake na ya wengine anaposemeshwa na wengine.
Kuna wakati hurudia maneno ambayo watu wengine wamezungumza.
Dalili nyingine ni mtoto kuzungumza kwa mtindo usio wa kawaida, mlezi au mzazi anashindwa kuelewa ikiwa mtoto ana furaha, hasira, au huzuni kutokana na sura yake au lugha ya mwili.
Kwa upande mwingine hupendelea kucheza peke yake kuwa mpweke muda mwingi.
Wazazi wanaihakikishia jamii kuwa usonji unaweza kutibiwa kwa kutumia tiba ya tabia ili kutengeza ujuzi wa kijamii, elimu maalumu shuleni na dawa kama vile vizuizi vya kumwepusha na kujiumiza.
Kuna baadhi ya familia zenye watoto wenye usonji, wanajaribu mlo maalumu au tiba mbadala, japo hakuna ushahidi kwamba njia hizi zinasaidia watoto hao.
Mbali na kuwa na changamoto hiyo wenye usonji wana mchango kwenye jamii, katika mambo mbalimbali kulingana na hali waliyonayo kwani wana uwezo wa kushiriki shughuli mbalimbali.
Wizara ya Afya imeanza kuongeza nguvu katika kuboresha upatikanaji wa huduma za utengamao kwa wenye usonji ikiwemo kuongeza idadi ya wataalamu wa huduma za saikolojiatiba.
La muhimu tusiwabague watoto hawa kutokana na hali zao kwani wote ni sawa kama wengine wenye utimamu kimaumbile na wanahitaji kupendwa, kulindwa na kufundishwa namna ya kumudu na kuendeleza maisha yao.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED