FAINALI za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), sasa zitafanyika kuanzia Agosti, mwaka huu huku wenyeji wakiwa ni Tanzania, Kenya na Uganda.
Nchi hizo tatu za Afrika Mashariki zilitangazwa kuwa mwenyeji wa fainali hizo baada ya kushinda maombi waliyowasilisha ambayo yalibeba jina la 'Pamoja Bid'.
Awali fainali hizo zinazoandaliwa na kusimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), zilitarajiwa kuchezwa kuanzia Februari Mosi hadi 28, mwaka huu.
Huku kukiwa na taarifa za maandalizi kufikia zaidi ya asilimia 90, lakini huu muda ambao umepatikana kufuatia michuano hiyo kusogezwa mbele utumike vyema kwa kuboresha kila kitu ambacho CAF ilielekeza.
Inafahamika CAF hutoa maelekezo maalumu kwa kila idara inayotarajiwa kuhusika ili kufanikisha fainali hizo kufanyika katika kiwango cha juu, hivyo tutumie 'mwanya' huu uliopatikana kukamilika mahitaji yote.
Kukamilisha maandalizi kwa upande wa miundombinu, isiwe tu katika maeneo ambayo yatatumiwa na timu, maofisa na wageni watakaokuwa nchini wakati huo wa mashindano, lakini tutumie pia kujifunza kufikia ubora wa kimataifa kwa kila huduma itakayotumika katika fainali hizo.
Wakati awali ukaguzi wa mwisho wa miundombinu ambayo ni pamoja na viwanja vya kuchezea mechi na vile vya mazoezi ulitarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu, sasa ukaguzi huo utafanyika Machi, huu ni wakati wa kuendelea kumaliza 'viporo' vya ukarabati unaohitajika.
Wataalamu na mafundi wanaofanya kazi katika maeneo hayo husika, hawatakiwi kupunguza kazi, wanatakiwa kuendelea kukamilisha majukumu waliyopewa na muda wa ukaguzi utakapofika, kila kitu kiwe kwenye ubora na viwango vya kimataifa kama mwongozo unavyoelekeza.
Wakati miundombinu ikiendelea kufanyiwa kazi, huu ni wakati mwingine kwa Idara ya Ufundi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na benchi la ufundi la Timu ya Taifa (Taifa Stars), kuhakikisha mapendekezo yake ya maandalizi yanafanyika kwa kiwango kile kile ilivyopendekeza.
Kutekeleza mambo yote ya msingi yaliyopendekezwa na Idara ya Ufundi pamoja na Kocha Mkuu wa timu hiyo, Hemed Morocco, kutakifanya kikosi kuwa imara kuelekea fainali hizo, kikosi chake kuimarika na kujiweka tayari na michuano kikiwa kamili.
Kuwa na kikosi imara, ndio njia pekee ya kutarajia kupata matokeo chanya, tutahitaji kuimarisha na kukiboresha kikosi cha Taifa Stars kwa vitendo ili kufikia ndoto za kuvuka hatua ya makundi kwa mara ya kwanza au kulibakisha Kombe la CHAN hapa Tanzania.
Wakati Serikali na TFF wakiendelea na mchakato wa kukamilisha mahitaji muhimu, pia huu ni wakati muhimu kwa mashabiki kujiandaa kwa ajili ya kujitokeza kwa wingi kuishangilia Taifa Stars katika mechi zake zote na kuonyesha uzalendo wa timu hiyo.
Kama ambavyo mashabiki hujitokeza kuziangalia timu zao wanapocheza kwenye viwanja vya nyumbani au husafiri kuzifuata klabu kuzishangilia zinapokuwa ugenini, huu ni mwaka wa kuweka rekodi kwa sababu fainali hizi za CHAN zinafanyika kwa mara ya kwanza hapa Tanzania.
Inafahamika na unatambulika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam ni moja ya viwanja ambavyo mashabiki hujaa, kama inawezekana wakati wa mechi za dabi, Tamasha la Simba Day na Siku ya Mwananchi, huu ni wakati mwingine wa kuwafanya wachezaji wa Stars wajisikie wanadeni la kupambana kusaka matokeo chanya.
Inawezekana kila mmoja kutekeleza majukumu yake na kuzifanya fainali za CHAN mwaka huu kuwa bora kutokana na wenyeji kuyabeba vyema mashindano hayo.
Tunamaliza kwa kuitakia maandalizi mazuri Taifa Stars.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED