WAJUMBE wa Mkutano Mkuu Maalum wa Taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), jana walimchagua kwa kishindo mwanasiasa mkongwe, Stephen Wasira, kuwa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Tanzania Bara. Wasira amechaguliwa kuziba nafasi ya Abdulrahman Kinana aliyeachia ngazi Julai, mwaka jana.
Kutokana na kuchaguliwa huko, Wasira pamoja na kuwa msaidizi wa Mwenyekiti wa Taifa wa Chama, Rais Samia Suluhu Hassan, upande wa Bara, pia ni Mwenyekiti wa Maadili wa chama kazi ambayo ni kuhakikisha kanuni na taratibu ndani ya chama hasa kwa wanachama zinafuatwa na kuheshimiwa.
Aidha, kwa nafasi hiyo, mwaka huu anatarajiwa kuwa na kazi nzito katika kupitia na kupitisha wanachama na makada wa chama hicho wanaotarajia kujitoa katika kinyang’anyiro cha ubunge na ujumbe wa Baraza la Wawakilishi.
Kuchaguliwa kwa mwanasiasa huyo mwenye wasifu mzito, hakukuwa kwa bahati wala upendeleo kwa kuwa uzoefu wake ndani ya chama na serikali unadhihirisha kwamba ana uwezo mkubwa. Kwa zaidi ya miongo mitano, Wasira ameshika nafasi mbalimbali zikiwamo katibu wa chama mkoa, mbunge, naibu waziri na waziri katika wizara mbalimbali zikiwamo nyeti. Pia amekuwa mjumbe wa Kamati Kuu ya halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM na NEC pia.
Kwa mantiki hiyo, Wasira anakijua chama ndani na nje kutokana na uzoefu wake kwenye nyadhifa hizo ndiyo maana anasifiwa kuwa ni ‘jembe’ na ameshiriki kikamilifu katika kampeni za uchaguzi za CCM na hatimaye kushinda. Sifa hizo na uzoefu wake vimewafanya hata wajumbe wa Mkutano Mkuu jana kumpongeza na kuonesha imani waliyo nayo kwake katika nafasi hiyo mpya.
Katika maneno yake baada ya kuchaguliwa, kiongozi huyo alitamka kwamba ana kazi mbili kubwa za kuanza nazo ambazo ni kukipigania chama na hatimaye kushinda katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu wa Rais, Wabunge, Wawakilishi na Madiwani, unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu, na hatimaye kushika dola.
Hakika hilo ni jukumu kubwa analoanza nalo ikizingatiwa kwamba mtangulizi wake, Kinana, ndiye alikuwa mtu muhimu katika kuchora ramani za ushindi wa CCM tangu alipokuwa Katibu Mkuu wa CCM hadi Makamu Mwenyekiti, kwa maana hiyo, Wasira atafuata nyayo za Kinana katika kuipatia CCM ushindi na yamkini wako baadhi ya wahafidhina watakaokuwa wakijaribu kumlinganisha na aliyemrithi.
Pamoja na hayo yote, CCM imempata mtu sahihi miongoni mwa wanachama wenye sifa katika kushika nafasi hiyo, hivyo hakuna kuweka wasiwasi kama anaweza kuvaa viatu vya Kinana.
Aidha, Wasira ana jukumu kubwa la kuhakikisha pamoja na ushindi kwa CCM katika uchaguzi mkuu na hatimaye kuendelea kukamata dola, ana kibarua kigumu katika kuhakikisha maadili ndani ya chama yanaimarishwa. Kumekuwa na tuhuma za rushwa kwa baadhi ya wanachama na makada wakati wa uchaguzi, hivyo akiwa mwenyekiti wa maadili, hilo ni jukumu hizo zinalomkabili.
Muda mwingi, viongozi wa juu wa chama hicho tawala wamekuwa wakikemea kukithiri kwa rushwa miongoni mwa wanachama wanapotaka nafasi za uongozi lakini hali bado imeendelea kuwa hivyo mwaka hadi mwaka.
Kwa hiyo Wasira kwa kushirikiana na wenzake, anapaswa kuondoa doa hilo ndani ya chama kwa kuwa limesababisha baadhi ya watu kukosa imani na hata kuona kuwa bila pesa mtu hawezi kupata uongozi.
Kazi hiyo anatakiwa kuanza mwaka huu hasa wakati wa mchakato wa kupata wagombea wa nafasi za ubunge, udiwani na uwakilishi katika uchaguzi mkuu. Rais Samia jana alionya baadhi ya makada kujipeleka majimboni kuweka mazingira ya ubunge huku wakifanya mikutano na kwamba majina yao yako mezani kwake.
Kwa mantiki hiyo, shauku kubwa ni kuona suala hilo la kuwashughulikia wanaofanya rafu majimboni, tena kabla ya wakati, linatimizwa kwa kufanya kazi na hatua kuchukuliwa dhidi yao.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED