Mwalimu kusajiliwa Wydad ni somo kwa wachezaji, marefa

Nipashe
Published at 10:37 AM Feb 10 2025
Selemani Mwalimu.

KWA miaka ya nyuma ni kitu ambacho hakuna mtu ambaye angeweza kutegemea kuona kikitokea kwa mchezaji kutoka klabu ya kawaida tu, isiyo na jina kubwa kama Fountain Gate kusajiliwa na klabu kubwa Afrika kama Wydad Casablanca ya Morocco.

Kwa masikio na macho yetu, tumeshuhudia straika wa Fountain Gate, Selemani Mwalimu, akisajiliwa na klabu hiyo ya nchini Morocco.

Amesajiliwa akiwa amecheza kwenye klabu yake kwa nusu msimu tu. Ikumbukwe kuwa hata alipoanza kuichezea timu hiyo, si wengi waliokuwa wakimfahamu kwani uwezo wake wa kupachika mabao ndiyo uliosababisha wengi kuanza kusaka historia yake.

Mwalimu alikuwa amesajiliwa na timu hiyo, akitokea KVZ ya Zanzibar, ambapo alimaliza msimu akiwa na mabao 20 na 'asisti' saba, kabla ya kusajiliwa na Fountain Gate.

Hadi anasajiliwa na Wydad Casablaca, alikuwa amepachika mabao sita, ingawa hakucheza mechi nyingi sana baada ya kufikisha idadi hiyo ya mabao.

Kusajiliwa kwa straika huyo kunaonesha kuwa Ligi ya Tanzania Bara ambayo kwa sasa inashika nafasi ya nne kwa ubora barani Afrika kwa mujibu wa Shirikisho la Kimataifa la Historia ya Soka na Takwimu (IFFHS), inafuatiliwa na klabu nyingi nje ya nchi.

Hii inaonesha wazi kwamba kwa sasa si lazima mchezaji aichezee Simba au Yanga ili aonekane na klabu kubwa za nje, badala yake anaweza kucheza klabu ndogo na uwezo wake ukaonekana kutokana na mawakala wengi wanaoifuatilia.

Hili sasa na liwe somo kwa wachezaji wa Kitanzania kuwa wanawenza kuonekana hata kama wanacheza kwenye klabu za madaraja ya kati, na kwamba jambo kubwa ni kuonesha uwezo na nidhamu mchezoni.

Mabao hayo sita ambayo, Mwalimu ameyafunga, hakuna hata moja alilofunga dhidi ya Simba au Yanga, wala kukamia mechi pindi alipocheza na timu hizo, badala yake yeye alikomaa na kucheka na nyavu kwenye mechi nyingine za Ligi Kuu na hatimaye kuonekana uwezo wake kambani.

Tunaamini hili ni somo kwa baadhi ya wachezaji ambao wanaona ili waonekane na kupata nafasi ya kucheza nje ya nchi zilizopiga hatua kisoka kama Morocco na kwingineko, ni lazima uzikamie Simba, Yanga au Azam, tena kukamia kwenyewe ucheze kibabe kama unataka kuondoka na shingo, mguu ama bega la wechezaji wa upinzani.

Ili mchezaji awe bora ni lazima acheze kwa kiwango hicho hicho tena kwa nidhamu kila mchezo na si kuchagua mechi.

Inawezekana kabisa, Mwalimu alikuwa akifuatiwa na maskauti bila yeye kufahamu, na kwa sababu yeye alikuwa akiweka tu mipira ndani ya nyavu bila kujali timu yake inacheza na nani, ndiyo iliyompa dili hilo.

Mara nyingi maskauti wana tabia ya kufuatilia wachezaji kwenye mechi nyingi tofauti tofauti na wanamfurahia mchezaji anayecheza kwa kiwango bora kwenye kila mchezo na si baadhi au kukamia kama ilivyo wengi nchini wanapocheza dhidi ya Simba, Yanga.

Kwa sasa ni fursa kwa wachezaji kufanya kweli bila kulazimika kwenda Simba, Yanga au Azam. Kingine ni kuacha tabia ya tamaa ya kuuza mechi. Kwani kuna madai ya baadhi ya wachezaji kuwa na tabia ya kuchukua pesa kwa timu pinzani ili kuhujumu timu zao. Hizo ni pesa za muda mfupi ambazo haziwezi kumsaidia siku zote, badala yake zinamfanya kuonekana kutokuwa na kiwango kizuri katika mechi kubwa.

Kwa wachezaji wenye tabia hizo  wanapaswa kuachana nazo na badala yake kupambana kwa ajili ya maisha yao ya baadaye kama ilivyokuwa kwa Mwalimu ambaye ni wazi sasa yupo kwenye malisho mazuri.

Hili si kwa wachezaji tu, bali hata kwa waamuzi, kwani kwa Ligi ya Tanzania fursa ipo ya kuchezesha mechi za kimataifa kwa sababu ligi yetu inatazamwa sana. Lakini kwa baadhi ya madudu tunayoshuhudia kwenye baadhi ya mechi wanatushushia hadhi.

Haipendezi kuona ligi ya nne kwa ubora Afrika, wachezaji wake wakianza kusajiliwa na klabu kubwa za Afrika Kaskazini kitu ambacho kilikuwa nadra sana hapo awali, lakini haina waamuzi bora wa kwenda kuchezesha kimataifa. 

Badala yake iwe ni Ahmed Arajiga tu ndiyo aaminike kwenye kuchezesha michezo hiyo, wakati miaka ya nyuma Tanzania ilisifika kwa kuwa na waamuzi bora kabisa  Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, kama kina Hafidh Ally, Abdulkadir Omar, Nassor Hamduni, na wengine ambao waliipatia nchi sifa, hivyo ni wakati sasa nao kudhaminisha ligi yetu kwa kuonyesha ubora wanapopewa nafasi kuchezesha mechi Ligi Kuu.