LIGI Kuu Tanzania Bara inatarajia kurejea tena leo baada ya kusimama kwa muda kupisha mashindano ya Kombe la Mapinduzi Zanzibar, michezo ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika.
Awali mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Tanzania Bara au hatua ya lala salama ilipangwa kurejea tena kuanzia Machi Mosi mwaka huu, ili kupisha kufanyika kwa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN).
Hata hivyo, Shirikisho la Mpira wa Miguu la Afrika (CAF), lilitangaza kusogeza mbele michuano hiyo hadi Agosti 2, mwaka huu na kupelekea Bodi ya Ligi Kuu (TPLB), kurudisha nyuma kalenda yake.
Bodi ya Ligi tayari imeshatoa ratiba mpya ambayo inaonyesha inaanza na mechi za viporo, leo kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam mabingwa watetezi wa ligi hiyo wakiwakaribisha Kagera Sugar kutoka Bukoba mkoani Kagera na kesho kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora wenyeji Tabora United wataikaribisha Simba.
Mbali na mashabiki na wadau wa soka 'ku-miss vibe' la Ligi Kuu Tanzania Bara, mechi hizo za viporo zinaonekana kama vile ndio za ufunguzi wa msimu kutokana na rekodi ambazo timu zinazokutana zimeweka.
Yanga imekuwa ikipata wakati mgumu ikikutana na Kagera Sugar hapa Dar es Salaam tofauti na wanapocheza ugenini huku Simba akisubiriwa kujibu 'kitendawili' cha kuizuia Tabora United kuvuna pointi kama ilivyofanya kwa mabingwa watetezi na Azam FC.
Mambo haya mawili yanaongeza mvuto wa kusubiriwa kwa michezo hiyo, lakini pia kukata kiu ya mashabiki na wadau wa soka ambao waliikosa burudani ya mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara kwa zaidi ya mwezi mmoja.
Wakati kila timu itaanza mzunguko wa pili, ingawa baadhi yao wameshacheza mechi 16, ikiwa na malengo yake, tayari baadhi zimeshajipambanua zina malengo yapi katika msimu huu unaoendelea wa mwaka 2024/2025.
Mpaka sasa kuna makundi matatu, kundi la kwanza ni zile ambazo zinaendelea kupambana kuwania taji na zinaonyesha wazi zina kiu kubwa ya kutwaa ubingwa kwa kila siku kujiimarisha na kujipanga kuvuna pointi tatu kwa sababu inaamini bado taji liko wazi.
Kundi lingine ni zile timu ambazo zimeshajidhihirisha zinahitaji pointi muhimu ili kujiweka mahali salama katika msimamo lakini pia zikihitaji kumaliza kwenye nafasi nne za juu na kukata tiketi ya kushiriki mashindano ya kimataifa yanayoandaliwa na CAF ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika.
Lakini pia kuna kundi ambao lenyewe malengo yake sasa ni kuvuna pointi na kujinusuru na janga la kushuka daraja kwa sababu kwao itakuwa ni miujiza zikibeba taji hilo, kutokana na kutokuwa na matokeo chanya katika mechi za mzunguko wa kwanza.
Hawa ndio hucheza kwa kukamia na wakati mwingine mechi zao hupoteza mvuto.
Katika soka lolote hutokea hasa pale michezo iliyobaki ni mingi, huu ni wakati wa viongozi, makocha na wachezaji kuongeza utulivu na hatimaye kusaka ushindi na kudhihirisha matokeo ya mzunguko wa kwanza yalitokana na 'kuteleza'.
Pia wachezaji kuonyesha kandanda safi sio tu kutaisaidia kupata matokeo chanya timu yao, ubora huo utawaongezea thamani wachezaji na kujiweka 'sokoni' kuelekea maandalizi ya msimu mpya.
Wachezaji kuonyesha nidhamu ndani na nje ya uwanja itawasaidia kuwaongezea mashabiki kujitokeza kwa wingi viwanjani kwa sababu wataamini wanakwenda kushuhudia vipaji na si vurugu au faulo ambazo hazistahili kutokea kwa wanamichezo.
Tunawakumbusha tunatarajia kushuhudia burudani na ufundi katika hatua ya mzunguko wa pili au lala salama.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED