Dawa wanaozuia maiti kisa deni sasa yamcheka

By Jenifer Gilla , Nipashe
Published at 08:59 PM Jan 31 2025
Chumba cha kuhifadhia maiti.
Picha: Mtandao
Chumba cha kuhifadhia maiti.

SERIKALI imesema itaanza kuchukua hatua kali kwa madaktari wanaozuia mwili kuchukuliwa na ndugu zao baada ya kushindwa kulipa gharama za matibabu, kinyume na maelekezo ya serikali.

Kadhalika, imetoa maelekezo kwa hospitali binafsi na za umma kuhakikisha wanatoa kwanza huduma kwa wagonjwa na si kuweka maslahi ya fedha mbele.

Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel, wakati akijibu swali la Mbunge wa Segerea, Bonnah Kamoli, lililokuwa likiuliza serikali inatoa tamko gani la wazi kwa wananchi wanaoshindwa kupata mwili kwa baada ya kushindwa kulipa deni.

Akijibu swali hilo, Dk. Mollel alisema serikali imekuwa ikipokea malalamiko ya ndugu kuchelewa kupewa miili kwa kushindwa kulipa madeni.

Dk. Mollel alisema kutokana na hilo, serikali itachukua hatua kwa daktari atakayesababisha usumbufu kama huo, ikiwa mwananchi anafuata taratibu zinazohitajika.

Alisema serikali ilishatoa maelekezo kwa vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini kupitia Waraka Namba Moja wa Mwaka 2021 wa kutozuia mwili na kuweka utaratibu wa kulipia gharama za matibabu na madeni ya miili.

 Naibu Waziri aliwaomba wabunge kuwaelimisha wananchi wao kufuata taratibu watakazopewa pale wanaposhindwa kulipa deni, kuwapo na rekodi ya waliosamehewa na kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za umma.

“Kwenye hospitali zote kumewekwa maofisa maendeleo ya jamii ili kukwepa hoja za wakaguzi, kwa sababu tusipofuata hivyo, watu wanaweza wakatumia mwanya huo kusema kuwa, wamesamehe kumbe fedha za umma zimetumika vibaya,” alisema.

Dk. Mollel alizielekeza hospitali zote kuhakikisha wagonjwa wa dharura hasa wajawazito wanapokwenda kufuata huduma, wanahudumia kwanza, kisha malipo yafuate baadaye ili kuepusha vifo vinavyozuilika.

Alisema katika huduma ya mama na mtoto, serikali ilipitisha bajeti ya Sh. bilioni 200, lakini mahitaji yake kwa mwaka ni Sh. bilioni 220, kwa hiyo kuna hatua nyingine zinafanywa ili kuhakikisha huduma hiyo inapatikana kwa uhakika.

Katika swali la msingi, Bonna alihoji hatua gani za kinidhamu zimechukuliwa kwa madaktari wanaoendelea kuzuia mwili kutokana na deni la matibabu kinyume na maelekezo ya serikali.

Akijibu swali hilo, Dk. Mollel, alisema miili huwa inazuiliwa na uongozi wa hospitali na wala si suala la madaktari.

“Na katika maeneo ambayo tumefanya ufuatiliaji ili kuchukua hatua za kinidhamu kwa viongozi husika, tumebaini ndugu wa marehemu ndio waliokataa kufuata utaratibu uliowekwa ili kuzuia hoja za ukaguzi na ndugu hao wakikimbilia kulalamika kwenye vyombo vya habari na kwa viongozi,” alisema.