Wanaojifungua watoto njiti sasa kicheko

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 08:14 AM Feb 01 2025
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde.
Picha:Mtandao
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde.

SERIKALI imeridhia hoja ya kuongeza muda wa likizo ya uzazi kwa mwajiriwa ambaye atajifungua mtoto njiti kwa kujumuisha na muda uliobaki kufikia wiki 40 za ujauzito huku baba akipewa siku saba za mapumziko.

Hoja hiyo imekuwa ikipigiwa chapuo kwa muda mrefu na Taasisi ya Doris Mollel, Mtandao Haki ya Afya ya Uzazi, TWPG, Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) ili kulinda ustawi na afya za watoto wanaozaliwa kabla ya wakati ambao wanahitaji muda wa kutosha wa uangalizi wa mama.

Majadiliano kuhusu hoja hiyo yalianza rasmi na wadau hao mwaka 2017 kisha kupelekwa Bungeni mwaka 2018.

Akiwasilisha jana bungeni maelezo ya Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Kazi namba 13 wa Mwaka 2024, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, alisema awali katika Muswada ilipendekezwa muda wa wiki 36 kama ukomo wa muda wa mtoto kutimia.

Hata hivyo, alisema baada ya majadiliano na kamati, serikali ilikubaliana na mapendekezo ya kuongezwa muda huo hadi kufikia wiki 40 na kuongeza muda wa likizo ya baba ambaye atapata mtoto njiti kuwa siku saba badala ya tatu.

Pia alisema kifungu kipya cha 34A kinapendekezwa kuongezwa ili kumwezesha mwajiri kumpatia mwajiriwa likizo bila malipo isiyozidi siku 30 ili kuweka mazingira mazuri yatakayomwezesha mwajiriwa kupata likizo bila malipo kutokana na majanga au dharura zinazoweza kujitokeza. 

Pamoja na hayo, kifungu cha 14 kinapendekezwa kubainisha aina ya mikataba ya muda maalum ili kuongeza wigo wa mazingira ambayo mtu anaweza kuajiriwa kwa mkataba wa kipindi maalum, ikiwamo mikataba ambayo mwajiriwa anaajiriwa kwa muda ili kuendana na ongezeko la wingi wa kazi, kutoa fursa kwa wahitimu wa vyuo ili kuwajengea uwezo na kufanya kazi nyingine  za misimu. 

Pia alisema mwajiri na mwajiriwa wanaweza kuingia katika makubaliano ya namna watakavyofanya kazi katika hali ya dharura inayoweza kuathiri uzalishaji mahali pa kazi wakati wa magonjwa ya milipuko na matukio ya dharura. 

Kadhalika, alisema kifungu cha 37 kimeweka masharti yanayozuia mwajiri kutoanzisha au kuendelea na shauri la nidhamu dhidi ya mwajiriwa pale ambapo mgogoro huo upo mbele ya Tume au Mahakama ya Kazi ili kuzuia uingiliaji wa mchakato kushughulikia migogoro.

Katika muswada huo, pia alisema fidia zimeainishwa kulingana na aina ya mgogoro na kuweka ukomo wa chini na wa juu wa fidia inayotolewa kwa mwajiriwa aliyeachishwa kazi isivyo halali huku Kifungu cha 41A kinapendekezwa kuongezwa ili kuweka masharti kuhusu afua kwa uvunjaji wa mkataba wa ajira ya muda maalumu.

Pia alisema kifungu cha 71 kimeweka masharti ya utaratibu wa kuanza kutumika kwa mikataba ya hali bora inayoingiwa na wakuu wa taasisi za umma. Lengo la marekebisho haya ni kuwianisha masharti ya sheria hii na utaratibu uliowekwa kwenye sheria zinazosimamia utumishi wa umma. 

Hata hivyo, alisema vyama vya wafanyakazi vimewezeshwa kwa pamoja kuingia mikataba ya hali bora na mwajiri au vyama vya waajiri kwa ajili ya kuanzisha majukwaa ya ushiriki wa waajiriwa mahali pa kazi.

Alisema kifungu cha 94 kimeweka masharti ya kuzuia wahusika wa mgogoro kuwasilisha maombi ya mapitio kwa maamuzi madogo ya Tume isipokuwa kama maamuzi hayo yana athari ya kumaliza mgogoro.

Akisoma maoni ya Kamati Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Fatuma Toufiq  alishauri serikali kuona namna ya kufanya maboresho katika sheria ili kuruhusu pia  wanaojifungua watoto wenye mahitaji maalum kama vile usonji, vichwa vikubwa, mgongo wazi, mdomo sungura, matundu kwenye moyo, seli mundu  ili kupewa likizo maalum ya uzazi pindi wanapojifungua.

Naye Mbunge wa Mchinga (CCM), Salma Kikwete aliwataka wanaume watakaopata likizo ya wiki moja baada ya wake zao kujifungua watoto njiti, kutotumia fursa hiyo kwa shughuli nyingine nje ya kuwasaidia wake zao.

AJIRA ZA WAGENI

Mavunde alisema Kifungu cha tisa cha Sheria ya Usimamizi wa Ajira za Wageni, Sura ya 436 kimeweka masharti ya kumtaka raia wa kigeni mwenye kibali cha kazi daraja A anayekusudia kujihusisha na kampuni nyingine anayomiliki hisa kupata idhini ya Kamishna wa Kazi badala ya kibali kingine cha kazi.

Alisema marekebisho hayo yanalenga  kuondoa usumbufu na kuweka mazingira bora ya uwekezaji kwa mwekezaji ambaye ni raia wa kigeni na baada ya kupata kibali cha kazi kwa kampuni moja hatahitajika kupata kibali kingine kwa kampuni  nyingine atakayomiliki hisa. 

Alisema kifungu cha 10 kimeweka masharti ya kuzuia urejeshwaji wa ada ya maombi ya kibali cha kazi ili kutoa ufafanuzi kwa waombaji wa vibali vya kazi kuhusiana na ada zinazolipwa wakati wa maombi.

Aidha, kifungu cha 12 kitawawezesha wakimbizi wenye hadhi stahiki kuendelea kufanya kazi  bila kubanwa na sharti la ukomo wa muda wa kibali cha kazi.

“Vilevile, kifungu hiki  kinarekebishwa ili kuwezesha maombi ya kuhuisha kibali cha kazi kuwasilishwa kwa Kamishna wa Kazi angalau miezi miwili kabla ya kuisha kwa muda wa kibali,” alisema.