SERIKALI iko katika hatua za mwisho za kutoa fedha kwa ajili ya vituo vya afya vya kimkakati katika majimbo na ukamilishaji wa maboma yaliyojengwa na wananchi.
Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, alisema jana bungeni jijini hapa wakati akitoa majibu ya nyongeza baada ya maswali ya wabunge kuhusu fedha za ujenzi wa vituo vya afya na ukamilishaji wa maboma ambayo yamejengwa kwa nguvu za wananchi katika sekta za afya na elimu.
“Tuko katika hatua ya mwisho kuanza utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa miundombinu ya kimkakati ya elimu na vituo vya afya msingi itakayokwenda sambamba na ukamilishaji wa maboma ambayo yamejengwa kwa nguvu ya wananchi,” alisema.
Awali Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Zainab Katimba, alilieleza Bunge kuwa serikali itatoa Sh. milioni 250 kwa kila jimbo kwa ajili ya kuendeleza miundombinu ya kutolea huduma za afya msingi, zikiwamo zahanati.
Alisema wabunge walijaza fomu za kuainisha maeneo ya kimkakati katika majimbo yao ili kujenga vituo vya afya kupitia fedha kutoka Serikali Kuu na mapato ya ndani kutoka halmashauri.
Aidha, alizihimiza halmashauri kupitia mapato ya ndani kutenga fedha kwa ajili ya kujenga miundombinu hiyo muhimu ya afya msingi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED